Mwalimu adaiwa kujiua kwa kujikata koromeo

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana lakini polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kilichomsibu mwalimu huyo.

Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mtenga wilayani Nkasi, Leonard Mwipugi (29) anadaiwa kujiua kwa kujikata koromeo akiwa nyumbani kwake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema chanzo cha kifo hicho bado hakijajulikana lakini polisi wanaendelea na uchunguzi ili kubaini kilichomsibu mwalimu huyo.

Hata hivyo, taarifa zilizotolewa na Mratibu wa Elimu, Kata ya Mtenga, Hebron Mwafungo zinaeleza mwalimu huyo amekutwa akiwa amekufa nyumbani kwake saa sita mchana juzi katika Kijiji cha Mtenga.

Alisema mwalimu huyo juzi alikwenda kazini kwake Shule ya Sekondari Mtenga na ilipofika saa tano asubuhi alirejea nyumbani na hakumkuta mkewe.

Alidai baada ya muda walipata taarifa kuwa mwalimu huyo amefariki dunia kwa kujikata koromeo.

Mwafungo alisema mwalimu huyo alikuwa akiishi na mdogo wake nyumbani hapo na alipofika, alimtuma mbali kidogo ya nyumba hiyo na baada ya mdogo wake kurudi aliona damu zikitoka ndani.

Alisema mdogo wake huyo alipochungulia aligundua kaka yake amejichinja koromeo na kutoa taarifa kwenye uongozi wa kijiji hicho.

Mwafungo alisema baada ya kumdodosa mdogo wa marehemu huyo alidai kuwa kaka yake siku za nyuma alikuwa na mgogoro na mkewe lakini ulikwisha ila anahisi kitendo cha mkewe kuondoka nyumbani na kwenda mjini Namanyere huenda jambo hilo lilimkera kaka yake na kuchukua hatua hiyo ya kujiua.