Mwalimu adaiwa kumpa mimba mwanafunzi

Muktasari:

  • Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima alitoa agizo hilo mbele ya kikao cha watumishi wa Serikali wa wilaya zote sita mkoani humo.
  • Kiongozi anayeona kuishi Mara ni adhabu atakiwa kuhama

Tarime. Ofisa elimu mkoa wa Mara, Emmanuel Kisongo ametakiwa kumchukulia hatua mwalimu wa shule ya msingi Namubi wilayani Bunda kwa madai ya kumpa mimba mwanafunzi (13) ambaye amejifungua watoto pacha.

Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima alitoa agizo hilo mbele ya kikao cha watumishi wa Serikali wa wilaya zote sita mkoani humo.

Kikao hicho kilichowahusisha wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala, wakuu wa idara na taasisi za Serikali kilifanyika wilayani hapa lengo kilikiwa ni kuwakumbusha watumishi wajibu wao na kutatua matatizo ya wananchi.

“Mwalimu mpaka sasa hajawajibishwa, badala yake akasingiziwa mwanafunzi kuwa ndiyo kambebesha mimba tena mtoto yatima asiye na baba wala mama. Kiongozi anayeona kukaa Mara ni adhabu ahame matukio ya ukatili yanatokea lakini viongozi hamchukui hatua,” alisema Malima.

Mkuu wa wilaya ya Bunda, Lyidia Bupilipili alisema uongozi wa wilaya umeshachukua hatua kwa mwalimu huyo (jina linahifadhiwa) kwa kumfikisha katika vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Ofisa elimu, Kisongo alisema mwanafunzi huyo alipewa mimba na mwalimu wake kisha akasingiziwa mwanafunzi wa darasa la saba (jina linahifadhiwa) kuwa ndiye aliyehusika kumpa ujauzito huo.

Kisongo alisema Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), William Kanon alisema mwanafunzi huyo tayari amejifungua watoto pacha.

Alisema tukio lingine limetokea Shule ya Msingi Nyamongo ambako mwanafunzi wa darasa la pili (8) alibakwa na mtu ambaye hajafahamika jina.

Kisongo alisema kuwa mama wa mtoto huyo (jina linahifadhiwa) aligundua mwanaye kubakwa Machi 22, 2017 na alikwenda kuripoti kituo cha polisi lakini hadi sasa anazungushwa bila kupata msaada wowote na hivyo taarifa kumfikia mkuu wa mkoa wa Mara.®