Friday, August 10, 2018

Mwalimu asema wabunge upinzani wamechapa kazi CCM ikawatamani

 

By Joseph Lyimo, Mwananchi jlyimo@mwananchi.co.tz

Babati. Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu amesema baada ya wabunge wa upinzani kufanya maendeleo kwenye majimbo yao CCM imeona jambo bora ni kuwarubuni ili wajiunge nayo.

Amesema baada ya CCM kuona wabunge wa upinzani wana kesi mbalimbali mahakamani lakini hawahukumiwi vifungo, wakaona kazi ni kuwarubuni wajiunge nayo.

Mwalimu aliyasema hayo juzi kwenye viwanja Mjini Babati mkoani Manyara wakati akimnadi mgombea udiwani wa Kata ya Bagara, Mathias Zebedayo.

Alisema chama hicho hakitetereki kutokana na baadhi ya wabunge wake kujiuzulu na kujiunga na CCM huku wakitoa sababu mbalimbali ambazo hazina mashiko kwa Watanzania wengi.

Alisema wao kama Chadema wataendelea kuwa kwenye chama hicho kwa kupigania ustawi wa demokrasia bila kuogopa chochote.

Mbunge wa jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema) alisema wananchi wa kata ya Bagara wana imani kubwa na mgombea wao Zebedayo hivyo watampigia kura za kutosha Agosti 12.

“Wananchi wengi ni waelewa na wametupima kutokana na miradi mbalimbali ya maendeleo tuliyofanikisha ikiwemo kwenye elimu, afya, maji na barabara,” alisema.

Zebedayo alisema anasubiri kuapishwa kwenye halmashauri ya mji wa Babati kwani wananchi wengi wanamkubali.

“Kura zangu zimeshajaa hadi sasa hivi mimi ninachosubiria ni kwenda kuapishwa na kuanza majukumu yangu ya kuwasemea wananchi wa kata ya Bagara,” alisema Zebedayo.

-->