VIDEO-Mwalimu atoa neno akimzika kiongozi Chadema

Muktasari:

Mwalimu amesema John amepoteza maisha akipigania haki ya kidemokrasia. 

Mafinga. Naibu katibu mkuu Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu ameongoza waombolezaji katika mazishi ya kiongozi wa chama hicho, Daniel John ambaye mwili wako uliokotwa ufukwe wa Coco akisema utamaduni huo ukiachwa unaandaa kizazi kitakacholipa kisasi.

John (37) aliyekuwa Katibu wa Chadema, Kata ya Hananasif mwili wake uliokotwa ufukweni mwa bahari baada ya kutoweka Februari 11.

Mwalimu ametoa kauli hiyo leo Februari 21,2018 alipotoa salamu za chama hicho kwenye msiba huo uliofanyika katika Kijiji cha Kitelewasi wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Amesema John amepoteza maisha akipigania haki ya kidemokrasia.

"Tunaamini John amefariki akitimiza majukumu yake ya kupiga kampeni kutafuta kura kwa ajili yangu na chama chake akipendacho," amesema Mwalimu aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Kinondoni katika uchaguzi mdogo uliofanyika Februari 17,2018.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa amesema kifo cha John kimetokana na shughuli zake za kisiasa.

Amewataka waombolezaji kutokata tamaa na kuendelea kupigania haki ya kidemokrasia ambayo John ameipigania hadi mwisho wa maisha yake.

Amesema ni jambo la msingi jamii kutambua kuwa hakuna mtu atakayeishi milele.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema, Patrick ole Sosopi amesema vijana wa chama hicho wamepata pigo lakini waendelee kupambana kudai haki ya kidemokrasia.

Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga amesema wanamuachia Mungu kilichotokea kwa John.