MwanaFA, AY waibwaga tigo mahakamani

Muktasari:

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya tigo kusimamisha utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala iliyoiamuru kampuni hiyo iwalipe fidia ya Sh2 bilioni kwa makosa ya ukiukwaji wa hakimiliki za wasanii hao.

Dar es Salaam. Wasanii wa muziki wa kizazi kipya, Hamisi Mwinjuma na Ambwene Yesayah ‘AY’ kwa mara nyingine wameibwaga mahakamani Kampuni ya Simu ya tigo baada ya kushinda pingamizi lao dhidi ya maombi ya kuzuia utekelezwaji wa hukumu ya awali.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali maombi ya tigo kusimamisha utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala iliyoiamuru kampuni hiyo iwalipe fidia ya Sh2 bilioni kwa makosa ya ukiukwaji wa hakimiliki za wasanii hao.

Kampuni hiyo ilifungua maombi mahakamani hapo ikiomba mahakama hiyo iamuru utekelezaji wa hukumu hiyo ya Mahakama ya Wilaya ya Ilala usimame kusubiri usikilizwaji na uamuzi wa rufaa yao waliyoikata kupinga hukumu hiyo.

Hata hivyo wasanii hao kupitia wakili wao, Albert Msando waliweka pingamizi dhidi ya maombi hayo ya tigo ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo, wakiiomba mahakama hiyo iyatupilie mbali, pamoja na mambo mengine wakidai kuwa yana kasoro za kisheria.

Akitoa uamuzi wake leo, Jaji Isaya Arufani amekubaliana na hoja za pingamizi la wasanii hao na akatupilia mbali maombi hayo ya tigo na hivyo kusubiri usikilizwaji wa rufaa yao.

Katika pingamizi lao, pamoja na mambo mengine Wakili Msando amedai kuwa maombi hayo ni batili kwa kuwa hawakutaja kifungu maalumu cha sheria kinachoipa mahakama mamlaka ya kuyasikiliza na kuyatolea uamuzi.

Pia Wakili Msando amedai kuwa maombi hayo yanakiuka sheria kwa kuwa yamewasilishwa bila kuwekwa dhamana mahakamani kinyume cha sheria na kanuni za mahakama, huku katika hoja ya tatu wakidai kuwa hati ya kiapo kinachounga mkono maombi hayo ni batili.

Wakili Msando alifafanua kuwa ofisa mtoa maombi aliyetoa kiapo hicho, Tumaini Shija hakueleza kama mambo aliyoyaeleza kwenye kiapo hicho ni kutokana na ufahamu wake mwenyewe au ni ya kuambiwa.

Hata hivyo Wakili wa tigo, Mbwambo amepinga hoja hizo akidai kuwa kutaja vifungu vingi kwenye sheria hakuathiri uhalali wa maombi hayo na kwamba suala la dhamana linaangaliwa wakati wa usikilizwaji wa maombi na si kabla ya kuanza kuyasikiliza.

Kuhusu suala la ubatili wa kiapo, Wakili Mbwambo pamoja na mambo mengine alidai kuwa hata kama mahakama ikiridhika kuwa kuna aya ambazo zina kasoro basi tiba yake ni mahakama kuamuru ziondolewe au kuamuru kufanyika kwa marekebisho.