Mwanafunzi IFM anaswa na bastola

Muktasari:

  • Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema juzi saa mbili usiku eneo la Mwenge, polisi walipata taarifa kuhusu tukio hilo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa na silaha hiyo na risasi sita ndani ya magazini.

Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam inamshikilia mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kwa tuhuma za kukamatwa na bastola aina ya Beretta ambayo alikuwa akijiandaa kuikodisha kwa Sh400,000 kwa wanaodaiwa ni majambazi.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema juzi saa mbili usiku eneo la Mwenge, polisi walipata taarifa kuhusu tukio hilo na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa akiwa na silaha hiyo na risasi sita ndani ya magazini.

Mambosasa alisema awali walipata taarifa kuwa kuna watu wanakodisha silaha kwa majambazi, ili wafanye uhalifu na kulipwa fedha hivyo uliandaliwa mtego eneo la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mwenge ambao ulifanikiwa kumnasa mtuhumiwa.

Inadaiwa alitaka kuikodisha kwa Sh400,000 , lakini alikuwa tayari iwapo angepata mnunuzi kuiuza kwa Sh2.5 milioni.

“Inavyoonekana silaha aliiba kwa baba yake ambaye naye si ya kwake. Tunataka kujua aliipata wapi hivyo tumewakamata wote,” alisema.

Alisema baada ya mtuhumiwa kuhojiwa alikiri kushirikiana na rafiki yake mkazi wa Tabata, Segerea ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Columbus State Community cha nchini Marekani, kukodisha silaha kwa wahalifu kwa nia ya kujipatia kipato.

Kamanda Mambosasa alisema kwamba upelelezi unaendelea kujua mmiliki halali wa silaha hiyo, kujua imekodishwa mara ngapi na matukio ilikotumika.