Mwanafunzi ajifungua shuleni

Muktasari:

  • Mwanafunzi huyo wa kidato cha tano alijifungua saa 10 alfajiri hali ambayo imezua utata kuhusu namna mwanafunzi huyo alivyokaa na ujauzito akiwa shuleni bila kugunduliwa.


Moshi. Mwanafunzi wa kidato cha tano wa Shule ya Sekondari Mawenzi ya Moshi amejifungua mtoto wa kike akiwa shuleni hapo.

Tukio hilo la aina yake lilitokea jana saa 10 alfajiri huku kukiwa na sintofahamu ya namna mwanafunzi huyo alivyokaa na ujauzito huo kwa miezi tisa bila kugunduliwa.

Lakini swali lingine linaloumiza vichwa ni namna mwanafunzi huyo alivyojiunga na shule hiyo akiwa mjamzito, wakati katika fomu za kujiunga na kidato cha tano ni lazima ziwe na taarifa ya daktari.

Kumpa mimba mwanafunzi ni kosa la jinai chini ya kifungu cha 60A cha Sheria ya Elimu sura 353, kama kilivyofanyiwa marekebisho na kifungu cha 22 cha sheria namba 2 ya mwaka 2016.

Kifungu cha tatu (3) cha sheria hiyo kinaeleza kuwa mtu yeyote atakayepatikana na hatia ya kumpa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Sheria hiyohiyo kifungu cha tano (5) inamtaka kila mkuu wa shule kuandaa taarifa ya kila robo mwaka ya matukio ya wanafunzi walioolewa au kupewa ujauzito na kuiwakilisha kwa kamishna wa elimu.

Taarifa kutoka ndani ya sekondari hiyo ambayo ni moja kati ya shule kongwe za Serikali nchini, zilidai mwanafunzi huyo alijifungua chooni alipokwenda kujisaidia na wanafunzi wenzake walimgundua.

Vyanzo vinadai kuwa mwanafunzi huyo alitoka bwenini usiku huo kwenda msalani ndipo alipojifungua na kumwacha mtoto chooni na baada ya wenzake kumshtukia, walitoa taarifa kwa mwalimu wa zamu.

“Alichukua muda mrefu huko chooni na hii iliwatia shaka wenzake na aliporudi na kumdadisi hakusema chochote, lakini baada ya kumbana alieleza kuwa amejifungua,” kilidokeza chanzo kimoja.

Mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alidai mwanafunzi huyo anayechukua mchepuo wa HKL, amelazwa katika Hospitali ya St Joseph huku hali ya mama na mtoto zikielezwa kuendelea vizuri.

Alipoulizwa kuhusu tukio hilojana, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Uhuru Mwembe alisema uchunguzi umeanza.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Koka Moita alisema tukio hilo halijaripotiwa katika kituo chochote cha polisi, lakini wamepata taarifa za kuwapo kwake.

Kamanda Moita alisema baada ya kupata taarifa hizo alituma askari kwenda Hospitali ya St Joseph na walielezwa kuwapo kwa mwanafunzi huyo, lakini hata hivyo alisema haonekani mahali alipo licha kutafutwa hadi wodini.