Mwanafunzi aliyetoweka apatikana Mafinga

Muktasari:

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Juma Bwire amethibitisha kupatikana kwa Nondo ambaye amesema yupo kituo cha polisi Mafinga akitoa maelezo ya tukio zima hadi kufika hapo

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (TSNP) na mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Abdul Nondo ambaye aliyepotea katika mazingira ya kutatanisha amepatikana wilayani Mufindi na sasa yupo Polis Mafinga akitoa maelezo.

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Juma Bwire amethibitisha kupatikana kwa Nondo ambaye amesema yupo kituo cha polisi Mafinga akitoa maelezo ya tukio zima hadi kufika hapo.

“Ni kweli amepatikana kijana anaitwa Abdul Nondo na yupo kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi akitoa maelezo jinsi alivyofika hapo,” amesema Kamanda Bwire.

Kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook kuliwekwa ujumbe kwenye akaunti ya Juma Dogan akifahamisha kuhusu kupatikana kwa mtu mjini Mafinga aliyejitambulisha ni mwanafunzi wa UDSM.

Taarifa za kupotea kwake zilielezewa leo Machi 7 na viongozi wa TSNP na ndugu wa Nondo walipozungumza na waandishi wa habari na kuelezea mazingira ya kupotea kwake.

Kadhalika taarifa zake zilielezwa na Rais wa Serikali ya Wanafunzi UDSM, Jeremiah Jilili kuwa taarifa za kupotea kwake zilienea baada ya kuonekana amejitoa kwenye makundi ya mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp.

“Tulichofanya ni kutoa taarifa kwa utawala,” alisema Jilili.

Kamanda wa Polisi Iringa ameahidi kutoa maelezo mengi zaidi leo Alhamisi