Mwanafunzi kidato cha nne akutwa amefariki

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tanga, Edward Bukombe

Muktasari:

RPC Tanga kutoa taarifa kesho

Tanga. Mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Old Tanga, Shufaa Mbughuni amekutwa amefariki dunia huku uso wake ukiwa umechubuliwa ngozi.

 

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Tanga, Edward Bukombe amesema mwili wa mwanafunzi huyo umekutwa leo Agosti 19, 2018 saa 9.40 alasiri katika mtaa wa Majani Mapana kata ya Nguvumali jijini Tanga.

 

Bukombe alisema taarifa kamili kuhusiana na tukio hilo ataitoa kesho mara baada ya

madaktari wa hospitali ya mkoa wa Tanga ya Bombo kuufanyia uchunguzi mwili wa mwanafunzi huyo.

 

"Ni kifo chenye utata hatuwezi kusema ameuawa au vinginevyo, tunasubiri

taarifa ya madaktari wa hospitali ya Bombo watakapouchunguza mwili huo (nami) nitawaeleza habari yote," amesema Bukombe.

 

Naye baba wa mwanafunzi huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa serikali ya mtaa

wa Majani Mapana, Salim Mbughuni amesema mwanaye aliwaaga wenzake juzi

saa 2.00 usiku kwamba anakwenda kijisomea lakini hakurudi kama ilivyo

kawaida yake.

 

“Aliwaaga wenzake kwamba anakwenda kujisomea na atarudi baada ya muda

mfupi lakini hakuweza kurejea hadi mwili wake ulipoonekana siku ya

pili mtaani hapa akiwa amekufa,”amesema Mbughuni.

 

Mmoja wa wanafunzi katika shule hiyo ambaye alijitambulisha kuwa ni rafiki wa Shufaa, Halima Juma alisema ameelezwa na wadogo zake kwamba kabla ya kuondoka alipigiwa simu ya kuitwa ndipo alipokwenda na hakurudi nyumbani.

 

“Mimi usiku ule nilipigiwa simu ya kuulizwa kama nilimwita Shufaa lakini ukweli ni kwamba sikumwita…leo hii rafiki yangu ameuawa kikatili namna hii inasikitisha sana”alisema  Juma.