Wednesday, January 11, 2017

Mwanakijiji alia na viongozi mbele ya DC

 

By Twalad Salum, Mwananchi tsalum@mwananchi.co.tz.

Misungwi. Mkazi wa Kijiji cha Iteja wilayani Misungwi, Ndohele Mathias amesema uongozi wao umekuwa ukiwatoza wafugaji faini wafugaji kati ya Sh500, 000 hadi Sh1,000,000 kwenye Hifadhi ya Ngitiri.

Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya Misungwi, Juma Sweda, mkazi huyo amesema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa na kimekuwa kikiwapa shida kukimudu.

Kufuatia lalamiko hilo alilolitoa mkazi huyo kwa niaba ya wenzake, Sweda ameuagiza uongozi wa Kijiji cha Iteja kupunguza kiwango cha faini wanachotozwa wafugaji kwa kuingiza mifugo kwenye hifadhi hiyo kutoka Sh500,000 hadi Sh100,000.

Akihutubia mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na wananchi kutoka vijiji vitatu vya Iteja, Mwamnga na Lubuga uliofanyika eneo la Viwanja vya Shule ya Msingi Iteja, pia amewataka viongozi wa Serikali za mitaa kuacha kutumia rasilimali za umma kujinufaisha.

“Badala ya kutumika kwa masilahi ya jamii inayohifadhi msitu wa kijiji, hifadhi imekuwa ikiwanufaisha viongozi ambao huwatoza faini wanaoingiza mifugo hifadhini na kujilipa posho. Tabia hii lazima ikome mara moja,” ameagiza Sweda.

Hifadhi hiyo imekuwa ikitunzwa na kijiji husika kama eneo maalumu la utunzaji miti na maliasili zingine za misitu na imekuwa kivutio cha watalii wa ndani.

-->