Mwanasheria ataka DC ashtakiwe kwa wadhifa wake

Muktasari:

Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Desdery Magezi anayesikiliza kesi hiyo alimuuliza wakili Faraji Mangula anayemwakilisha Ole Lapoy iwapo anakubali ombi hilo.

Chunya. Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Edwin Kaisi anayewatetea Mkuu wa wilaya hiyo, Rehema Madusa na Ofisa Mifugo, Julius Ng’wita katika kesi ya madai ameiomba mahakama kumpa muda ili kufafanua hoja ya kutaka wateja wake washtakiwe kwa nyadhifa zao na si kama watu binafsi.

Kesi hiyo ilifunguliwa Machi mosi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Chunya na Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) wilayani Chunya, Shang’ai ole Lapoy akiwashtaki kama watu binafsi huku akitaka alipwe fidia ya Sh100 milioni baada ya kushinda kesi iliyokuwa ikimkabili.

Ole Lapoy anadai kudhalilishwa baada ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu saa 48 kwa amri ya mkuu wa wilaya Julai, 2017 na baadaye kushtakiwa mahakamani kwa kosa la kuwazuia watumishi wa Serikali kutimiza majukumu yao wakati wa mpango wa kupiga chapa mifugo.

Kaisi kwa niaba ya Wakili Faraja Msuya anayewatetea Madusa na Ng’wita, jana aliiomba Mahakama kumuongezea muda wa siku sita ili kukamilisha hoja zake akidai wateja wake walikuwa wanatekeleza majukumu ya kiserikali.

Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Desdery Magezi anayesikiliza kesi hiyo alimuuliza wakili Faraji Mangula anayemwakilisha Ole Lapoy iwapo anakubali ombi hilo.

Mangula anayeshirikiana na wakili Ezekiel Kihiyo kumuwakilisha Ole Lapoy walikubaliana na ombi la mwanasheria huyo.

Wakili Mangula alisema akipata ufafanuzi wa hoja hizo ataiomba mahakama kuwajibu wadaiwa ndani ya siku 14.

Hakimu aliahirisha shauri hilo hadi Mei 24 atakapotoa uamuzi wa ombi hilo.

Machi 13, Mwanasheria wa Halmashauri ya Chunya, Bilali Bilago kwa niaba ya wakili Msuya aliwasilisha hoja tatu mahakamani kutaka wadaiwa washtakiwe kwa nyadhifa zao badala ya mtu binafsi.

Wakili huyo alipinga madai ya fidia ya Sh100 milioni kwa wateja wake akidai walipaswa kudaiwa kwa nyadhifa zao na si wao binafsi kwa kuwa Rehema ni mkuu wa wilaya, hivyo angewakilishwa na mwanasheria wa Serikali na Julius Ngwita ni ofisa mifugo angewakilishwa na mkurugenzi wa halmashauri.

Alidai Ole Lapoy si mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji wilayani Chunya na kwamba, madai ya kulipwa fidia ya Sh100 milioni sio ya kweli. Ole Lapoy alipofikishwa mahakamani hapo alidaiwa kutenda kosa Julai 27, 2017 katika kitongoji cha Izumbi kilichopo kwenye Kijiji cha Sangambi wilayani Chunya, ambako alimzuia ofisa mifugo wa wilaya kupiga chapa mifugo.

Licha ya upande wa mashtaka kuwasilisha mashahidi watatu, Ole Lapoy aliachiwa huru na mahakama baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka.