Mwanasheria mkuu aombwa kusaidia haki itendeke

Moshi. Familia ya Juma Hamis aliyefariki dunia Julai 28 baada ya kushambuliwa kwa kipigo mjini Moshi imemuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kuingilia kati sakata hilo.

Baba mdogo wa marehemu, Salim Juma alisema Aprili 25, Juma alipigiwa simu kwa ajili ya kwenda kutengeneza pikipiki, lakini alipofika eneo hilo alikamatwa na vijana watatu waliodaiwa kumshambulia kwa kipigo.

Alisema vijana hao walimlazimisha akiri kuhusika na tukio la ubakaji.

Salim alisema Juma alipopata nafasi alikimbia lakini walimpigia kelele za mwizi, ndipo akakimbizwa na kundi la watu wakidhani ni mhalifu wakaanza kumpiga.

“Alipata madhara sehemu za kichwani, kwa mujibu wa CT Scan ubongo ulikuwa umecheza. Pia alivunjwa uti wa mgongo pamoja na shingo,” alisema.

Alifafanua kuwa walilazimika kutoa taarifa polisi kuhusu tukio hilo, lakini hawakupata ushirikiano hadi mgonjwa wao akapoteza maisha.

“Ndiyo maana namuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali anisaidie kuhakikisha haki inatendeka kujua sababu ya kuuawa kwa mwanangu na watuhumiwa wakamatwe wafikishwe mahakamani,” alisema.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro (RPC), Hamis Issah alisema vijana waliohusika kujeruhi walikamatwa na baadaye waliachiwa kwa dhamana.

Alisema mtuhumiwa aliyempigia simu Juma akimtaka aende kutengeneza pikipiki amekamatwa na atafikishwa kwenye vyombo vya dola.