Nuzulack Dausen apeta tuzo za mwandishi bora Afrika

Muktasari:

Ameshinda tuzo hizo katika masuala ya nishati na miundombinu

Addis Ababa-Ethiopia. Mwandishi mwandamizi wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Nuzulack Dausen ameshinda tuzo ya mwandishi bora Afrika wa masuala ya nishati na miundombinu katika tuzo za umahiri wa habari Afrika za Zimeo zilizotolewa jana Alhamisi usiku jijini hapa.

Zimeo ambazo zimetolewa kwa mara ya tatu sasa ni tuzo maarufu katika tasnia ya habari barani Afrika sambamba na tuzo za CNNMultichoice ambazo zimekuwa zikitolewa kila mwaka.

Tuzo hizo za Zimeo hutolewa na shirika linaloshughulikia ukuaji wa tasnia ya habari Afrika ya African Media Initiative (AMI) yenye makazi yake jijini Nairobi, Kenya na kudhaminiwa na mashirika mbalimbali ya kimataifa yakiwemo Unesco, Kamisheni ya Uchumi ya Afrika ya Umoja wa Mataifa (ECA) na Shirika la Habari la Al-Jazeera.

Katika kipengele cha nishati na mazingira, Dausen alikuwa akichuana na wanahabari Jeffrey Moyo ambaye huandikia Shirika la Habari la Thomson Reuters na The New York Times na Femi Asu wa gazeti la The Punch la nchini Nigeria.

"Kwanza namshukuru Mungu kwa tuzo hii ya heshima katika maisha yangu ya uandishi wa habari na nawashukuru viongozi na wafanyakazi wenzangu wa MCL kwa kunijenga kitaaluma na kunitia moyo kwa kila nachojaribu kukifanya.

"Pia nawashukuru familia yangu kwa kunipa moyo wa kufanya kazi kwa bidii na kukubali kunikosa kwa muda napokuwa katika majukumu ya kazi nje ya Dar es Salaam na wasomaji ambao maoni yao hunijenga zaidi," amesema Dausen.

Dausen, ambaye ni mhariri wa habari za takwimu wa MCL, amesema uhuru wa habari na uandishi mahiri wa habari unaochambua masuala kwa kina utasaidia kuchochea maendeleo Tanzania na duniani kwa ujumla kwa kuainisha fursa na kutoa majibu ya changamoto zinazoikabili jamii.

Habari iliyompa ushindi Dausen inahusu namna wakazi wa vijiji vya Namikango A na B wilayani Nachingwea mkoani Lindi Tanzania walivyotumia fursa ya umemejua kupata mwanga na kukabiliana na umaskini. Habari hiyo ilichapwa katika gazeti dada la The Citizen zaidi ya miezi miwili iliyopita.

Akizungumzia vigezo vya utoaji tuzo hizo, Jaji Mwandamizi katika tuzo hizo Dk George Nyabuga wa Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) amesema walizingatia vigezo vingi vya kihabari vikiwemo uhalisia wa wazo la habari, mpangilio wa hoja na umahiri wa kueleza habari hiyo ikaeleweka na wananchi wa kawaida.
Vigezo vingine ni namna mada husika inavyowagusa wananchi, matumizi ya takwimu na uzingatiaji misingi ya habari ya usawa, weledi, na ukweli.

"Haikuwa kazi rahisi kuchambua mamia ya kazi za wanahabari Afrika nzima hadi kupata washindi wetu leo, " amesema Dk Nyabuka.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa AMI, Erick Chinje amesema ili vyombo vya habari viwe na msaada kwa watu wa Afrika ni lazima tasnia ya habari iboreshe utendaji wake kwa kuripoti na kuchambua masuala yanayogusa wananchi.
"Mchango wa AMI umekuwa katika kuandaa mipango ambayo itawasaidia wanahabari kuongeza uwezo wao kitaaluma na mbinu nyingine zitakazofanya wawe bora zaidi. Tuzo za Zimeo zitawatambua wanahabari waliofanya vyema katika kuripoti sekta muhimu katika maisha ya watu," amesema Chinje.

Baadhi ya wanahabari walioshinda tuzo hizo jana usiku ni Dorcas Wangira kutoka Kenya, Ridwan Dini-Osman kutoka Ghana na Jay Caboz wa Afrika Kusini aliyeibuka mshindi wa jumla wa tuzo hizo.