Mwandishi aliteta na mwanamfalme kabla hajauawa

Muktasari:

Kwa mujibu wa mtandao wa Uturuki wa Yeni Safak, mwandishi huyo alizungumza na mwanamfalme huyo mwenye umri wa miaka 33 ambaye alijaribu kumshawishi kurudi nyumbani

 


London, Uingereza. Mwanamfalme Mohammed bin Salman alizungumza kwa simu na mwanadishi wa habari Jamal Khashoggi akimtaka arejee Riyadh muda mfupi kabla ya kuuawa na kikosi maalum, mtandao mmoja wa Uturuki umedai.

Khashoggi, 59, imeripotiwa kwamba alikamatwa na kundi la maofisa 15 wenye nguvu kutoka Saudi Arabia punde baada ya kuingia jengo la ubalozi mdogo Istanbul saa 7.00 mchana Oktoba 2.

Kwa mujibu wa mtandao wa Uturuki wa Yeni Safak, mwandishi huyo alizungumza na mwanamfalme huyo mwenye umri wa miaka 33 ambaye alijaribu kumshawishi kurudi nyumbani.

Mtandao huo umedai kwamba Khashoggi alikataa akihofia kukamatwa na kuuawa nchini Saudi Arabia. Baada ya hapo, mtandao ukaripoti Khashoggi aliuawa kwenye ubalozi mdogo.

Habari za mtandao zimekuja kipindi ambacho Televisheni ya Uturuki imedai maofisa wa Saudia walichoma ushahidi katika bustani ya ubalozi huo siku ambayo Khashoggi aliuawa.

Televisheni ya A Haber ambaye ina uhusiano na serikali ilitangaza kwamba wanaume watatu wakiwa wamevalia suti walionekana wakichoma nyaraka kwenye pipa wakidai kwamba walikuwa wanateketeza nyaraka zinazohusiana na kifo cha mwandishi.

Mtangazaji wa TV anasikika akisema: “Hii ni njia ya zamani ya kuteketeza nyaraka. Hatumii njia ya kuchanachana. Ni kama vile wanataka kuteketeza kabisa kila ushahidi unaohusiana na Khashoggi.”

Watumiaji wa mtandao wa Twitter walichunguza na kubaini kwamba video ile ilipigwa kwa kutumia drone za upelelezi za Uturuki. Serikali ya Uturuki haijatoa maoni yake kuhusu picha hiyo ya video.

Pia usiku, ofisa chanzo kimoja cha intelejensia kutoka Saudia na kingine kutoka Uturuki vililiambia shirika la habari la Reuters kwamba ofisa msaidizi wa ufalme wa Saudi Arabia aliyefukuzwa kutokana na jukumu aliokuwa nalo katika mauaji ndiye alikuwa akiongoza shughuli kwa kutumia mawasiliano ya Skype.

Saud Al-Qahtani, ambaye alikuwa anasimamia mtandao wa kijamii wa mwanamfalme, inadaiwa alimtukuna mwandishi wa habari baada ya kukamatwa kwenye ubalozi kabla ya kukiamuru kikosi cha wauaji “nileteeni kichwa cha mbwa”.

Alifukuzwa kazi Jumamosi na kisha akafanywa kuwa mwenyekiti wa Shirikisho la Saudia la Usalama wa mtandaoni, Upangaji na Drone, jukumu alilowahi kuwa nalo awali.