Mwandishi aliyepiga picha mauaji ya Mwangosi afariki

Mwandishi wa habari wa Tanzania Daima aliyepiga picha ya mauaji ya Mwangosi, Joseph Senga wakati wa uhai wake

Muktasari:

Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo, Neville Meena alisema jana kuwa Senga (pichani) atazikwa nyumbani kwao Kwimba, mkoani Mwanza.

Dar es Salaam. Wakati Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, ikimhukumu Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Pasificus Simon kifungo cha miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daud Mwangosi juzi, siku hiyo hiyo mwandishi wa habari wa Tanzania Daima aliyepiga picha ya mauaji hayo, Joseph Senga amefariki dunia.

Mhariri Mtendaji wa gazeti hilo, Neville Meena alisema jana kuwa Senga (pichani) atazikwa nyumbani kwao Kwimba, mkoani Mwanza.

Alisema Senga alifariki dunia juzi usiku nchini India alikokuwa akipata matibabu ya ugonjwa wa moyo.

Meena alisema taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kutoka India kuja nchini zinafanyika.

Pia, Meena alisema taratibu nyingine za kuagwa na kusafirishwa mwili huo kwenda Kwimba zitajulikana leo.

Enzi za uhai wake, Senga ndiye alipiga picha mauaji ya Mwangosi kwa kulipuliwa na bomu Septemba 2, 2012 katika Kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kazi kwenye ufunguzi wa tawi la Chadema.

Chadema wamlilia

Akitoa salama za rambirambi, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alisema wamepokea kwa masikitiko na mshtuko taarifa za kifo cha Senga.

“Wanachama na viongozi tumejikuta tumeishiwa maneno ya kusema kuhusu kifo cha Senga hasa siku ambayo kimetokea.

“Kitendo hicho kimedhihirisha jambo moja kubwa kuwa Senga alikuwa shujaa wa demokrasia na haki,” alisema Makene.

Alisema picha za mauaji hayo zinapatikana kwenye mitandao ya kijamii.