Mwandishi wa Mwananchi ahojiwa polisi

Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Kituo cha Dodoma, Sharon Sauwa

Muktasari:

Mahojiano hayo yamefanywa leo Februari 22, 2018  na Inspekta Beatrice aliyesafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma aliyesaidiwa na askari mwingine wa mkoani hapa.

Dar es Salaam. Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Kituo cha Dodoma, Sharon Sauwa amehojiwa na polisi kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam.

 

Mahojiano hayo yamefanywa leo Februari 22, 2018  na Inspekta Beatrice aliyesafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma aliyesaidiwa na askari mwingine wa mkoani hapa.

 

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto amesema hana taarifa hiyo na kwamba apewe muda wa kufuatilia.

 

Alipofuatwa baadaye amesema wanaoweza kuzungumzia suala hilo ni polisi makao makuu na si yeye.

 

Alipotafutwa, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Barnabas Mwakalukwa amemtaka mwandishi amtafute Kamanda Muroto.

 

 Hata alipoambiwa kwamba tayari kamanda huyo amepatikana na kusema kuwa yeye si msemaji na kwamba wanaostahili kusema ni polisi makao makuu, Mwakalukwa amesisitiza kuwa Muroto ndiye anapaswa kusema amemkamata kwa sababu gani.

 

“Lakini pia tusubiri kama kweli wamemhoji au kumkamata na wakaamua kumleta Dar es Salaam. Endapo atafikishwa Kinondoni nijulishe nitakwambia umfuate kamanda wa mkoa huo, Kamishna Salome Kaganda na iwapo atafikishwa ‘central’ utaenda kwa Mambosasa,” amesema.

 

“Wakati mwingine mnaweza kufikiri kuwa amekamatwa kwa sababu ya masuala ya kiuandishi mnasahau mwandishi naye ni binadamu kama wengine, anaweza fanya kosa lolote la jinai kama wizi na mengine, hivyo tusubiri wakimleta utajua ukweli,”amesisitiza Mwakalukwa.

 

Hata hivyo, Mwakalukwa amemtaka mwandishi aongee na mtuhumiwa mwenyewe ili aeleze kilichomsibu kwa kuwa ni mtu mzima na kwamba, hajanyang’anywa simu yake ya mkononi hivyo ana mawasiliano.

Sharon alikamatwa jana kwa kile kinachodaiwa kuwa amefanya makosa ya kimtandao na kuamuriwa kuacha simu yake ya mkononi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

 

Mwandishi huyo alihojiwa kwa takribani saa mbili kuanzia saa 3:35 hadi 5:24 asubuhi na kuachiwa bila masharti yoyote huku akielezwa kuwa kama watamhitaji watamuita tena.