Mwandishi wa kujitegemea mkoani Njombe ‘akamatwa na polisi’

Muktasari:

Kibiki aliyevamiwa usiku wa kuamkia leo Februari 22, 2018 huandikia gazeti la Raia Mwema na mitandao mbalimbali.

Makambako. Mwandishi wa habari wa kujitegemea, Emmanuel Kibiki amevamiwa nyumbani kwake mjini Makambako, Mkoa wa Njombe na kukamatwa na watu waliojitambulisha kuwa polisi.

 

Kibiki aliyevamiwa usiku wa kuamkia leo Februari 22, 2018 huandikia gazeti la Raia Mwema na mitandao mbalimbali.

 

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, John Temu alipoulizwa kuhusu tukio hilo leo na MCL Digital amesema huenda Kibiki amekamatwa na taasisi nyingine, si polisi.

 

“Kuwepo kituo cha polisi haina maana kwamba amekamatwa na polisi. Kwamba ameachiwa au hajaachiwa hilo sina uhakika nalo, maana polisi hatuna taarifa za kukamatwa kwake,” amesema.

 

Akizungumza leo Februari 22, 2018 na MCL Digital, mke wa Kibiki, Tobina Kibiki amesema walishangaa kuona mlango unagongwa saa sita usiku na walipofungua walikutana na kundi kubwa la askari wakiwa na magari mawili.

 

Amesema askari hao walijitambulisha na kutaka kufanya upekuzi jambo lililowafanya wakubali kupekuliwa japo awali mume wake aligoma.

 

Tobina amesema baada ya upekuzi huo askari hao waliondoka na mume wake.

 

“Walikuja askari wengi japo sikuwahesabu ila mpaka tuliogopa. Ilikuwa kama saa sita usiku na kwa sababu walipekua ndani na kuchukua baadhi ya nyaraka, ilifika hadi saa tisa alfajiri,” amesema.

 

“Walisema wamekuja kutokana na maelekezo toka juu kuwa Kibiki ameandika habari za uchochezi.”

 

Leo alfajiri mke wa Kibiki alipozungumza na MCL Digital aliahidi kuwa asubuhi angeenda kituoni kumtazama mumewe ili kuhakikisha kama kweli yupo.

 

Saa tano asubuhi leo, Tobina amethibitisha kuwa mumewe yupo kituoni hapo akiendelea na mahojiano.