Mwanzo wa mwisho utawala wa Makonda Dar?

Muktasari:

Sasa kuna dalili kuwa ile hali ya kumwagiwa sifa na Rais John Magufuli, iliyochangia kung’arisha nyota yake, imebadilika.

Dar es Salaam. Matukio ya hivi karibuni yanayozunguka utendaji wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kauli zilizotolewa na viongozi wakuu wa nchi kuhusu mwenendo wake, zimeibua shauku kubwa kuhusu hatima ya kiongozi huyo kijana.

Sasa kuna dalili kuwa ile hali ya kumwagiwa sifa na Rais John Magufuli, iliyochangia kung’arisha nyota yake, imebadilika.

Makonda aliuteka moyo wa Rais Magufuli ambaye hakusita kumsifia na kumhakikishia nafasi yake kila mara upepo wa kisiasa unapovuma dhidi yake.

Nyota ya Makonda ilianza kung’aa tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Februari, 2015.

Ujasiri wake wa kutaka kufanya mambo makubwa ulimshawishi Rais Magufuli kutamka hadharani kuwa Makonda amejihakikishia nafasi ya ukuu wa mkoa hata kabla ya uteuzi rasmi alipokutana na wazee wa Dar es Salaam, Februari 14, 2016.

Akionyesha imani kubwa aliyokuwa nayo kwa Makonda, Rais Magufuli alisema: “Ninajua sijateua wakuu wa mikoa, ma-DC na wakurugenzi. Nimefanya kwa makusudi ili niendelee kuwachambua vizuri… lakini angalau mheshimiwa Makonda umeshajihakikishia angalau utakuwemo.”

Mwezi mmoja baadaye, Machi 13, 2016, Rais kupitia kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mussa Iyombe ambaye alikaimu nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi, alitangaza rasmi kumteua Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.

Tangu aliposhika ukuu wa wilaya ya Kinondoni, Makonda alijipambanua kuwa mtu anayetaka kufanya mambo makubwa ambayo ni alama ya kumbukumbu ya uongozi wake.

Katika kutimiza hilo, alijikuta akitengeneza marafiki kwa upande mmoja na maadui wengi kwa upande wa pili.

Alianza utawala wake kwa kufanya ziara za kushtukiza huku jina lake likipamba vichwa vya habari vya magazeti kwa staili yake ya kuwasimamisha na wakati mwingine kuwaumbua viongozi wa umma asioridhishwa na utendaji wao.

Hata hivyo, alikutana na jaribio kubwa dhidi ya utawala wake pale sauti zilipovuma kutoka kila kona zikitaka awajibishwe kwa madai ya kutumia ‘vyeti vya kughushi’ huku baadhi wakitaka Rais Magufuli atengue uteuzi wake.

Lakini baada ya kimya cha muda mrefu, Rais alifunga mjadala huo kwa kutamka kuwa wananchi wasipoteze muda kuzungumzia mambo ya mitandaoni na kumtaka mteule huyo kuendelea “kuchapa kazi”.

Ni Makonda huyu ndiye aliyeweka makubaliano na wamiliki wa vyombo vya usafiri kuanzia Machi, 2016 kuwa walimu wa sekondari na msingi mkoani Dar es Salaam, hawatalipa nauli katika daladala.

‘Uvamizi’ wa chombo cha habari.

Zamu hii akiongoza kundi la askari waliovalia sare, walidaiwa kuvamia Kituo cha Televisheni cha Clouds na kuibua shutuma kubwa kutoka kwa wamiliki wa vyombo vya habari na watetezi wa haki za binadamu.

Wengi waliamini kitendo hicho kisingemwacha salama, lakini matarajio yao yaliishia kuwa ndoto ya mchana.

Makonda alisimamisha tena nchi pale alipotangaza kuanzisha kampeni ya kupambana na dawa za kulevya iliyoshuhudia wafanyabiashara na wanamuziki maarufu nchini wakihojiwa na kushtakiwa kwa tuhuma za kujihusisha na biashara hiyo haramu.

Aprili mwaka huu, Makonda alizua mjadala mwingine mpya baada ya kutangaza kuwa ana mkakati wa kupita nyumba kwa nyumba kuwapima wanaume wote tezi dume. Kabla ya hapo, alianzisha kampeni ya usafi katika Jiji la Dar es Salaam na wafanyabiashara wote bila kujali ni biashara ya aina gani walitakiwa kutofungua maeneo yao kabla ya saa nne asubuhi siku za Jumamosi akilenga kufanyika kuruhusu usafi wa mitaa.

Upepo wa kisiasa ulibadilika na kuvuma dhidi yake kwa mara ya kwanza baada ya Rais Magufuli kuagiza kupigwa mnada kwa makontena 20 yenye thamani ya Sh1.2 bilioni ambayo Makonda aliagiza na kutaka yasamehewe kodi.

Kabla ya agizo la Rais Magufuli, Makonda alifanya kila jitihada ikiwamo ya kuwachukua baadhi wa walimu na waandishi wa habari na kuwapeleka kwenye Bandari Kavu kuona samani zilizokuwamo ndani makontena hayo aliyodai ni masaada kutoka kwa Watanzania waishio Marekani wanaojulikana kama Six Region Diaspora Council.

Tayari Makonda alikwishaandika barua kwa Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango akitaka vifaa hivyo visamehewe kodi baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutangaza orodha ya mali walizokusudia kupiga mnada yakiwamo makontena hayo.

Baada ya TRA kusisitiza kuuza makontena hayo kwa mujibu wa sheria, Makonda aliibukia katika ibada mjini Ngara mkoani Kagera na kutahadharisha kuwa atakayeyanunua atalaaniwa na Mungu.

“Nimekwenda katika ibada ya Jumapili katika Kanisa la Anglikakana mjini Ngara, nimefanya ibada maalumu kuhakikisha makontena hayo hayapati wateja kwa kuwa naamini Mungu alinipa kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam,” alisema.

Kauli hiyo ilikuwa kama kuchokoza nyuki. Siku iliyofuata, Dk Mpango alikwenda kukagua makontena hayo na kuagiza yapigwe mnada akisema, “Kamishna piga mnada mara ya kwanza, ya pili na ya tatu kadri sheria inavyoruhusu. Hata mimi ningekuwa na hela ningekuja kununua tuone hiyo laana itatoka wapi.”

Wachambuzi wanadai kuwa ujasiri wa Dk Mpango dhidi ya Makonda, hata kama alikuwa anasimamia sheria haukuwa wa kawaida.

Rais Magufuli ndiye aliyehitimisha siku 20 za mjadala wa makontena ya Makonda pale alipoagiza yalipiwe ushuru huku akionya viongozi kuwatumia watumishi wa umma kwa masilahi binafsi.

“Umesikia hili sakata la Dar es Salaam, eti Mkuu wa Mkoa ameleta makontena, ameambiwa alipe kodi, kwa nini asilipe kodi? Alihoji Rais Magufuli alipozungumza na madiwani, watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Chato, mkoani Geita.

“Sasa ukichukua makontena kule, umezungumza na watu wengine, labda na wafanyabiashara, unasema ni makonetna yako, halafu ukasema tena labda ni ya walimu, wala hata shule hazitajwi, maana yake nini? Maana yake si unataka kutumia walimu ulete haya makontena?” Alihoji Rais.

Ingawa kwa upande mmoja, kauli ya Rais Magufuli ilihitimisha mjadala wa ‘makontena ya Makonda’, kwa upende mwingine iliashiria mwanzo wa mjadala mpya juu ya hatima yake kisiasa.

Mjadala huu wa hatima ya Makonda ulikolezwa na Katibu Mkuu wa CCM alipokaririwa na Gazeti la Raia Mwema akisema Makonda alipaswa kuwashirikisha wenzake tangu hatua za awali, kwa kuwa Serikali ni moja.

Kwa mujibu wa Raia Mwema, Dk Bashiru Ally alimnyooshea kidole Makonda akikumbusha kuwa Dar es Salaam ni mmojawapo ya mikoa isiyotekeleza vyema Ilani ya CCM kutokana kufanya kazi bila ushirikiano.

Alimuonya Makonda juu ya tabia yake ya kuwaita wakazi wa Dar es Salaam, wananchi (Mkoa) wangu. “Na hii habari ya Dar es Salaam ya Makonda, hakuna Dar es Salaam ya Makonda, ni Dar es Salaam chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda.”

“Kuna wakati namsikia anasema wananchi wangu, nani kamwambia anao wananchi wake? Hakuna wananchi wako. Hakuna kiongozi anamiliki wananchi, ni wananchi wenzangu.”

Je, kauli za Rais Magufuli, Dk Mpango na Dk Bashiru zitamwacha Makonda Salama?

Makonda amekataa kuzungumza lolote pale Mwanachi ilipotaka kauli yake juu ya wanaotaka ajitafakari na kufanya uamuzi baada ya sakata la makontena.

“Yaani unanunua vocha na kupoteza muda wako kutaka tujadili hilo?!” alisema Makonda kabla ya kukata simu.