Mwenge wazidi kuchanja mbuga

Muktasari:

  • Amour aligoma kuzindua mradi wa ujenzi wa shule hiyo iliyopo wilayani Lushoto akiwashutumu wasimamizi kuijenga chini ya viwango.

Mwenge wa Uhuru ulitua mkoani Tanga wiki hii na kisha kiongozi wake, Amour Hamad Amour kugoma kufungua mradi wa ujenzi wa Shule ya Msingi Mkundi ya Mbaru akiiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuuchunguza, hatimaye umezindua miradi saba yenye thamani ya Sh1.9 bilioni.

Amour aligoma kuzindua mradi wa ujenzi wa shule hiyo iliyopo wilayani Lushoto akiwashutumu wasimamizi kuijenga chini ya viwango.

Hata hivyo, ukiwa katika mwendelezo wa ziara yake, mwenge huo umezindua miradi hiyo Halmashauri ya Bumbuli iliyotekelezwa kwa nguvu za wananchi na Serikali. Katika mchanganuo, Sh3 milioni za miradi hiyo zimetolewa na wananchi, halmashauri imetoa Sh37 milioni huku Serikali kuu ikitoa Sh1.88 bilioni.

Baadhi ya miradi iliyozinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi ni nyumba ya mganga wa zahanati ya Mbuzi, miundombinu Sekondari ya Mbelei na ofisi ya Kata ya Dule B.

Miradi mingine ni ujenzi wa jengo la upasuaji Kituo cha Afya Mgwashi na miundombinu ya mradi wa maji.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Simon Mwaiteleke alisema kwamba katika halmashauri hiyo tayari vikundi 40 vya vijana na wanawake wajasiliamali vimenufaika na mikopo tangu mwaka 2013.