Mwenyekiti UWT aanza kwa gia ya Rais Magufuli

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Gaudensia Kabaka

Muktasari:

  • Akizungumza jana katika hafla ya kumkaribisha iliyoandaliwa na UWT Mkoa wa Dodoma, Kabaka alisema umoja huo una mali, miradi, nyumba, viwanja na ardhi ambavyo thamani yake inapanda kila siku

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Gaudensia Kabaka amewapa miezi miwili viongozi wa ngazi zote wa jumuiya hiyo kuwasilisha taarifa ya mali.

Akizungumza jana katika hafla ya kumkaribisha iliyoandaliwa na UWT Mkoa wa Dodoma, Kabaka alisema umoja huo una mali, miradi, nyumba, viwanja na ardhi ambavyo thamani yake inapanda kila siku.

Desemba 12, akifungua mkutano wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Rais John Magufuli aligusia mali za umoja huo, yakiwamo majengo na kutamka kuwa zinatumika ovyo.

Alitoa mfano wa jengo la umoja huo lililopo Dar es Salaam ambalo halijulikani linakusanya mapato kiasi gani kila mwaka, kauli ambayo Kabaka ameibeba na kuibwaga UWT, akitaka maelezo ya mali za umoja huo.

“Muorodheshe mali zote za jumuiya na ndani ya miezi miwili nipate taarifa. Umoja una mali nyingi zilizopo ngazi ya kitaifa, mkoa, wilaya na kata. Ninataka kupata taarifa zake katika kipindi hicho,” alisema Kabaka.

Alisema ni lazima UWT ijipange na kufanya utekelezaji wa mpango kazi walioutengeneza.

Kuhusu rushwa, Kabaka alisema katika uchaguzi uliomweka madarakani hakuna mgombea aliyetoa rushwa ili achaguliwe, hivyo kuwataka wanawake hao kuepuka rushwa.

“Rushwa si sifa ya kumchagua kiongozi mzuri. Kiongozi atakayechaguliwa kwa rushwa hawezi kuheshimiwa wala kuwaheshimu wana jumuiya kwa sababu fedha ndiyo imemchagua,” alisema.

Alisema katika uchaguzi wa jumuiya hiyo mwaka 2022 atahakikisha hakuna kitu kinachoitwa rushwa ili kupata viongozi.

Aliwataka wanachama wa jumuiya hiyo kuisimamia Serikali, kufuatilia huduma za jamii na wakibaini kuna mambo hayaendi sawa, waishauri Serikali.

Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dodoma, Neema Majule aliahidi kutekeleza maagizo hayo kwa kuorodhesha mali za umoja huo zilizopo wilayani na mkoani.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.