Mwigulu: Msihoji uamuzi wa Rais

Muktasari:

  • Awashauri wapiga kura wake kupuuza maneno ya upotoshaji

Iramba. Mbunge wa Iramba Magharibi, Dk Mwigulu Nchemba amesema aliacha kazi nzuri Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ili kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo.

Dk Mwigulu alisema hayo juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika tarafa ya Kinampanda kuwahamasisha wananchi kushiriki utekelezaji miradi ya maendeleo.

Alisema wananchi wasinung’unike wala wasihangaike kutafuta sababu ya kupumzishwa nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani.

“Ndugu zangu wala msivunjike moyo, msianze kuhoji imekuaje au itakuwaje. Kumbukeni wakati wa michuano ya Kombe la Dunia huko Urusi, mchezaji mzuri anafunga goli lakini anatolewa akapumzike. Wachezaji wa aina hii walikuwa hawanuni wala hawalalamiki. Mimi sijanuna wala sitanuna kwa sababu moja kubwa, nayo ni kwamba uamuzi wa Rais ni sahihi na wa kawaida,” alisema.

Mbunge huyo aliwataka wananchi kupuuza maneno ya wapotoshaji, hivyo watambue uamuzi wa Rais ni halali na unalenga kuboresha utendaji wa Serikali yake.

Dk Nchemba alisema sasa atakuwa na muda wa kutosha kushirikiana kwa karibu na wananchi na kwa uhuru mpana katika kutatua changamoto za sekta mbalimbali.

Alisema kwa vile ana afya njema, nguvu za kutosha na elimu nzuri atashirikiana na wananchi ili jimbo hilo liwe la kupingwa mfano kwa maendeleo.

Awali mbunge huyo alikagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Afya Tarafa ya Kinampanda. Alichangia mifuko 400 ya saruji na nondo 100.

Awali, akimkaribisha mbunge huyo, diwani wa Kinampanda, Justas Makala aliwataka wananchi kumuunga mkono mbunge wao kwa kushiriki kikamilifu utekelezaji wa miradi ikiwamo ya sekta ya afya.

“Mbunge wetu anawatumikia vyema wananchi wake kwa kuhamasisha na kusaidia kwa hali na mali miradi ya maendeleo. Hivyo, hatuna budi kumuunga mkono kwa kushiriki kwa vitendo kutekeleza miradi ya maendeleo yetu wenyewe,” alisema.