Nchemba atunukiwa Shahada ya Uzamivu

Rais mstaafu Jakaya Kikwete akimtunuku Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Uchumi katika masuala ya fedha za kigeni katika mahafali ya 47 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Muktasari:

Rais mstaafu Jakaya Kikwete ndiye aliyewatunuku shahada wahitimu hao.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ni miongoni wa wahitimu waliotunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Uchumi katika masuala ya fedha za kigeni katika mahafali ya 47 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Katika mahafali yaliyofanyika leo Jumamosi Novemba 18,2017 wahitimu 79 akiwemo Mwigulu wametunukiwa shahada hiyo katika fani mbalimbali.
Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais mstaafu Jakaya Kikwete ndiye aliyewatunuku shahada wahitimu hao.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala amesema wahitimu waliotunukiwa leo ni wa awamu ya kwanza.
Amesema kwa kuzingatia uwiano wa jinsi kwa wahitimu wa mwaka huu, asilimia 30 ni wanawake na asilimia 70 ni wanaume.
“Tunawapongeza wahitimu kwa kutimiza vigezo stahiki vya kutunukiwa digrii katika fani na ngazi mbalimbali,” amesema Profesa Mukandala.
Amesema anaamini wamewaandaa vya kutosha kwa ajili ya kujumuika na jamii ya Watanzania katika kutafuta maendeleo.