Mwigulu amnadi mgombea udiwani Babati

Aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba

Muktasari:

Michael anayechuana na Christopher Chiza wa CCM katika uchaguzi huo unaofanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Kasuku Bilago kufariki dunia Mei 26, alisema hoja yake kubwa itakuwa kuimarisha ulinzi shirikishi kutokana na kuibuka kwa matukio ya utekaji na uhalifu.

Babati/Kigoma. Wakati aliyekuwa waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba akiibukia wilayani Babati mkoani Manyara kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Bagara (CCM), Nicodemus Tlaghasi, mgombea ubunge wa Chadema katika Jimbo la Buyungu, Eliya Michael anavuta subira kuanza kampeni.

Michael anayechuana na Christopher Chiza wa CCM katika uchaguzi huo unaofanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Kasuku Bilago kufariki dunia Mei 26, alisema hoja yake kubwa itakuwa kuimarisha ulinzi shirikishi kutokana na kuibuka kwa matukio ya utekaji na uhalifu.

Katika kampeni zilizofanyika juzi jioni kwenye viwanja vya Mtaa wa Mji Mpya mjini Babati, Mwigulu alikuwa pamoja na mbunge wa Babati Vijijini (CCM), Jitu Vrajlal Soni.

Mwigulu aliwaomba wakazi wa eneo hilo kumchagua Tlaghasi ili kumuunga mkono Rais John Magufuli katika juhudi zake za kufanikisha maendeleo ya wananchi, hasa miradi mikubwa anayoianzisha nchini. “Maendeleo yote yanayofanyika nchini ni utekelezaji wa ilani ya CCM, hivyo msipotoshwe na wapinzani hapa Babati wanaojinadi kuwa watatekeleza mambo ya maendeleo, hizi barabara za lami na miradi ya maji ni kazi ya Rais Magufuli,” alisema.

Alisema wananchi wa kata hiyo hawana sababu ya kupoteza muda kumchagua mgombea udiwani ambaye hatokani na CCM kwa sababu hawezi kuwa daraja la kuwapeleka kwenye maendeleo.

Naye Jituson alisema wananchi wa Kata ya Bagara walifanya kosa siku za nyuma, hivyo wasirudie tena kosa hilo kwa kumchagua mgombea wa upinzani.

“Tlaghasi aliona mbali kwa kujitoa Chadema na kujiunga na CCM, hivyo huu ndiyo wakati wa kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kumchagua mgombea wa CCM kwenye ngazi ya udiwani,” alisema Jituson.

Tlaghasi aliwaomba wananchi wa Bagara wampe kura za kishindo ili aweze kuendelea kuwatumikia akiwa kwenye chama tawala.

Mgombea huyo alijiuzulu udiwani akiwa Chadema na kujiunga na CCM ambayo imempitisha kuwania tena nafasi hiyo

Ulinzi wawatesa Chadema

Kwa upande wake, Michael anayegombea Jimbo la Buyungu kwa tiketi ya Chadema, alisema matukio ya utekaji yamesababisha athari nyingi katika shughuli za kiuchumi na kuwafanya wananchi kuishi maisha ya hofu.

Eliya, ambaye ni diwani wa Kata ya Gwarama, alisema tangu alipochaguliwa mwaka 2015, vifo 36 vimetokea katika kata hiyo vikihusiana na matukio hayo ya utekaji nyara na uhalifu mwingine.

“Baada ya kuona takwimu hiyo nilihamasisha watu wa Kata ya Gwarama kufanya ulinzi shirikishi na kuweka zamu ya doria, tangu kipindi hicho hakujatokea tukio lolote kwenye kata hii,” alisema.

“Wananchi wengi wanaamini kuwa jukumu la ulinzi ni la polisi, lakini wanasahau kwamba polisi wetu ni wachache, hivyo lazima tushirikiane kulinda mipaka na maeneo yetu ya makazi,” alisema.

Kuhusu kuchelewa kuanza kampeni, Eliya ambaye ni diwani kupitia Chadema, alisema ilitokana na msimamizi wa uchaguzi kuchelewa kuunganisha ratiba za vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo.

Aomba kura kwa kupiga magoti

Wilayani Kyela mkoani Mbeya mgombea udiwani wa Kata ya Mwanganyanga (Chadema), Alfredy Andembwise alilazimika kupiga magoti kuwaomba wananchi kumchagua, huku akieleza vipaumbele vyake vitatu.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa ufunguzi wa kampeni zake juzi jioni kwenye viwanja vya Mtaa wa Mkombozi, Andembwise alivitaja vipaumbele vyake kuwa ni kuendeleza miradi ya kuunganisha barabara za mitaa, kuhamasisha wananchi kupata kituo cha afya na kufungua akaunti maalumu ya kata kwa ajili ya kusaidia vijana na wanawake.

Nyongeza na Godfrey Kahango