Mwijage: Mazingira ya biashara yakiwa mabaya msitulaumu, mtuombee

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage

Muktasari:

Wakati wafanyabiashara nchini wakiendelea kulia na Serikali juu ya mazingira rahisi ya ufanyaji biashara, Waziri wa Viwanda na Biashara amesema jambo hilo likishindikana asilaumiwe yeye wala Rais bali aombewe ili lifanikiwe haraka

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage amesema mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini yasipokuwa mazuri asilaumiwe yeye wala Rais bali aombewe ili aweze kufanikisha kwa haraka.

Mwijage amesema hayo leo Oktoba 15, 2018 wakati akizindua kiwanda cha kuzalisha vilainishi vya mitambo na mashine cha Lake Lubes kilichopo Kigamboni jijini hapa.

Amesema suala la kuboresha mazingira ya biashara ni maelekezo ya Rais John Magufuli hivyo atajitahidi kuboresha ikiwa ni pamoja na kupunguza mamlaka za usimamizi na kusisitiza kitabu cha mwongozo cha Blue print ndiyo suluhisho.

"Mambo ya uboreshaji wa mzingira ya biashara ni maelekezo ya Rais yasipokuwa mazuri msimlaumu Rais, hata mimi msinilaumu bali mniombee ili tuweze kwenda haraka,"amesema Waziri Mwijage.

Aidha katika tukio hilo Mwijage amewapigia debe waajiriwa wa kampuni mbalimbali akisema wafanyakazi wanatakiwa kulipwa mishahara minono ili wachagie katika kodi za Serikali kupitia makato ya mishahara na manunuzi wanayofanya.

"Wafanyakazi walipwe vizuri hata kama kodi ya kampuni itapungua (Cooperate Tax) Serikali itaendelea kupata kodi kutokana na makato ya mishahara na wananchi kuwa na uwezo wa manunuzi," amesema Mwijage.