Mwijage abeba zigo la viwanda kwa mawaziri wengine Dodoma

“Siwezi kukubali kupoteza uwaziri. Kila mtu atabeba mzigo wake,”

Dar es Salaam.  Siku moja baada ya Rais John Magufuli kuwatolea uvivu mawaziri watatu kuhusu kasi ndogo katika utekelezaji wa maagizo ya Serikali, mmoja wao, Charles Mwijage amesema wiki hii atakutana na mawaziri wenzake mjini Dodoma na baada ya hapo atatoa uamuzi wa hatua gani zitafanyika.

Waziri huyo wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji amesema hatua alizoanza kuchukua awali ni kuwaita wamiliki wa viwanda hivyo na kuzungumza nao ili kujua ni kwa nini hawaviendelezi viwanda.

Mawaziri wengine walioingia kwenye mtego wa Rais Magufuli ni Dk Charles Tizeba (Kilimo, Chakula na Mifugo), kwa kutokufika katika Kiwanda cha Tanga Fresh kutatua matatizo waliyo nayo na Profesa Makame Mbarawa ambaye ni Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa kushindwa kutoa uamuzi kwa mwaka mmoja sasa kuhusu ujenzi wa ‘flow meters’ bandarini.

Rais Magufuli alionyesha kuchukizwa na mawaziri hao juzi alipokuwa akizungumza na wananchi kwa nyakati mbalimbali jijini Tanga ambako alielezea kushangazwa kwake jinsi viwanda vilivyobinafsishwa kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita lakini haviendelezwi.

Alisema vipo ambavyo walipewa baadhi ya wawekezaji kwa urafiki wa viongozi waliopita hivyo akamuagiza Waziri Mwijage kuvifuta bila kuangalia sura. “Sasa wewe waziri usiangalie sura za marafiki wa wenzako waliotangulia, nataka kuona kiwanda kimefutwa, nimezungumza mara nyingi, sitaki kukaa narudia hili kila siku,” alionya.

Akihojiwa jana kuhusu agizo hilo katika Kituo cha Redio Clouds FM, Waziri Mwijage alisema Ijumaa wiki hii atakutana na mawaziri wenzake kujadili ni viwanda gani mfu, kwa nini na hatua gani zichukuliwe na baada ya hapo atatoa uamuzi.

Kuhusu Rais kurudia mara kadhaa agizo hilo, alisema hatua alizoanza kuchukua awali ni kuwaita wamiliki na kuzungumza nao ili kujua ni kwa nini hawaendelezi.

“Watalaamu na makatibu wakuu wanakaa tarehe 10, mawaziri wanakaa Alhamisi na Ijumaa kule Dodoma, kama mawaziri hawataonekana, nitafanya kazi na nitasema mawaziri wameamua... na baadaye tutatoa utaratibu tukishirikiana na wakuu wa mikoa,” alisema.

Mwezi uliopita akiwa mjini Morogoro, Rais Magufuli aliwaagiza wafanyabiashara walionunua viwanda wakati Serikali ilipoamua kuvibinafsisha na kushindwa kuviendeleza wavirudishe.

Pia Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa mikoa kufanya tathmini kwenye mikoa yao kubaini viwanda ambavyo vilibinafsishwa lakini vimekaa kwa muda mrefu bila kuendelezwa.

Alipoulizwa kuhusu utekelezaji wa agizo la Rais kuhusu flow meter, Profesa Mbarawa alimtaka mwandishi kuzungumza na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) inayoshughulikia suala hilo kwa sasa.

Alipotafutwa, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema suala hilo lipo katika taratibu za ununuzi na kwamba hatua hiyo imeanza Machi mwaka huu na baada ya kukamilika,  hatua ya kutafuta mkandarasi itafuata kwa ajili ya kuanza kazi.

“Suala la manunuzi ni siri, huwezi kuambiwa ni hatua gani zimeshafanyika au gharama zitakuwaje, subiri tukimaliza hatua hii tutaeleza,” alisema Kakoko.