Mwijage apokea wawekezaji kutoka Ukrain

Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage

Muktasari:

Mwijage amesema ugeni huo utakuwa na manufaa kwa nchi kuelekea Tanzania ya viwanda kutokana na nchi hiyo kufanya vizuri katika viwanda na uundaji wa mashine.

Dar es Salaam. Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage amepokea ugeni kutoka nchini Ukraine katika maonesho wa viwanda yanayoendelea jijini hapa.
Mwijage amesema ugeni huo utakuwa na manufaa kwa nchi kuelekea Tanzania ya viwanda kutokana na nchi hiyo kufanya vizuri katika viwanda na uundaji wa mashine.
"Nitanunua mashine kutoka kwao, nitazibomoabomoa na nitaziunda hapa nchini upya, sifichi," alisema Mwijage.
Mwijage alisema walivutiwa na kuja kuuza dawa nchini ila akawataka si kuja kuuza dawa badala yake waje wajenge viwanda vya dawa.
Aliongeza kuwa mbali na dawa pia wameonesha nia ya kuja kuuza matunda ila kwanza ni lazima watengeneze viwanda.
Mwijage ambaye yupo kwenye mwendelezo wa maonyesho hayo yatakayoisha Desemba 11 alitumia fursa hiyo pia kuwatia moyo wenye viwanda vidogo kupitia Sido  wanasema ukiwa na vyerehani vinne tayari ni kiwanda.
"Nimeona mashine Sido ya sabuni kwa milioni nane inazalisha miche 1,400 na malighafi tunazo sasa umeme umefika vijijini hivyo kupitia maonesho hayo wananchi watajua mengi zaidi," alisema Mwijage.
Mwenyekiti wa kikundi Kazi Disabled Group, Hadija Mwaole ambacho kinajumuisha walemavu 19 kufanya shughuli za ufumaji na ushonaji kwa kutumia mashine za cherehani na mikono alisema bado soko lina changamoto.
Bi Hadija alitaja changamoto nyingine inayowakuta ni suala la usafiri kuwahi maeneo ya kazi kutokana na ugombaniaji wa daladala.
"Tunamuomba Rais John Magufuli atuwekee usafiri maalum kwa ajili ya kuwahi maeneo ya kazi ili kufanya shughuli za viwanda kama alivyohamasisha na kuzalisha bidhaa nyingi," alisema Bi Hadija.
Kadhalika alitoa wito kwa walemavu wengine kujitoa na kufanya kazi na si kuomba omba barabarani, ambapo wao walianza kuwa nane mpaka  sasa 19.