Mwili wa Akwilina kuwasili Rombo kesho asubuhi

Muktasari:

  • Mwili wa mwanafunzi huyo umeagwa leo Februari 22, 2018 katika viwanja vya chuo hicho na ndugu kuelekea wilayani Rombo kwa mazishi.


Rombo. Mwili wa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini unarajiwa kuwasili kesho alfajiri Februari 23, 2018 katika Kijiji cha Marangu kilichopo Kata ya Marangu Kitowo wilayani Rombo.

Mwili wa mwanafunzi huyo umeagwa leo Februari 22, 2018 katika viwanja vya chuo hicho na ndugu kuelekea wilayani Rombo kwa mazishi.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa leo nyumbani kwa baba wa marehemu inaeleza kuwa, baada ya mwili huo kufika utapelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Theresia Parokia ya Olele saa 3:40 asubuhi.

Inaeleza kuwa waombolezaji wataanza kutoa heshima za mwisho saa 4:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana.

Ratiba hiyo inaeleza kuwa atakayeongoza ibada ya mazishi nyumbani kwa wazazi wa marehemu kuanzia saa 7:00 mchana hadi saa 8:30 ni Paroko wa kanisa hilo,  Evans Mavumilio.

Baada ya misa hiyo, watu mbalimbali watatoa salamu za rambirambi hadi saa 9:00 alasiri ambapo wataelekea makaburini kwa ajili ya kuuhifadhi mwili wa mwanafunzi huyo.