Mwili wa Gamba bado uko mikononi mwa polisi

Muktasari:

Gamba ambaye wakati mwingine alikuwa akiitwa kwa jina la ‘mwanangu’ na marafiki zake wa karibu kutokana na uchechi wake amekuwa akielezewa na wengi kama mwanahabari aliyefanya kazi kwa weledi na kila alipopita aliacha alama ya matumaini


Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa mtangazaji wa Idhaaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW), Isaac Muyenjwa Gamba unatarajiwa kuwasili nchini Jumapili  baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa kitabibu kubaini kile kilichosababisha kifo chake.

Mwili wa mwanahabari huyo aliyekutwa amefariki duniani nyumbani kwake mjini Bonn bado uko mikononi mwa polisi na madaktari.

Taarifa kutoka Bonn zinasema hadi sasa polisi hawajasema lolote na huenda wakatoa ripoti yao wakati wowote kuanzia kesho.

Kwa mujibu wa kaka mkubwa wa marehemu, Julius Gamba mazishi yake yamepangwa kufanyika Bunda lakini tarehe yenyewe bado haijafahamika.

Amesema  mwili wa marehemu utaagwa Jumatatu ijayo Lugalo na kisha utasafirishwa kueleka Bunda, Musoma kwa ajili ya mazishi.

“ Kama kila kitu kitaenda sawa tunatarajia kupokea mwili wa mpendwa wetu Jumapili na siku inayofuata tutamwagia pale Lugalo na ndipo tuendelee na safari ya kwenda kuzika” amesema

 

 Gamba aliyejiunga Dw mwaka 2015 akitokea ITV/ Radio One alikuwa mmoja wasoma habari mahiri na kuendesha vipindi vya habari na matukio na kifo chake kimeshtua wengi kuanzia katika jengo la Dw mpaka maeneo mengine ambako alifahamika kutokana na ucheshi wake.

Katika kipindi cha muda mfupi baada ya kuwasili Bonn, Gamba aliyehitimu shahada ya uandishi wa habari katika Chuo Kikuu cha Tumaini, alifahamika maeneo mengi ya jiji la Bonn kutokana na ucheshi wake na wepesi wa kufahamiana na watu.

Katika taarifa yake kuhusiana na kifo hicho, DW ilisema imepoteza mtangazaji mahiri aliyemudu kazi yake kuanzia kwenye habari, ripoti za matukio duniani hadi michezo.

Tokea DW ilipoanza kutangaza Ligi Kuu ya Ujerumani(Bundesliga), Isaac alijiunga na kikosi cha watangazaji wengine kuwapa burudani wasikilizaji wa kabumbu. Pambano la mwisho alilotangaza ni mchuano kati ya Augsburg na Borussia Dortmund.

Tangu habari za kifo chake zilipojulikana ,waliomfahamu katika maeneo mbalimbali ya jiji la Bonn wamekuwa wakielezea masikitiko yao, wakishtushwa na taarifa hizo.

 

Alhamisi usiku vijana wa asili tofauti walionekana mitaani wakizungumza kwa huzuni kubwa kuhusu msibahuu.

DW imesema kufariki kwake ni pengo kwa Idhaaya Kiswahili na waandishi wa habari na watangazaji wa taasisi hiyo Ujerumani na Tanzania kwa ujumla.

Maisha ya utangazaji aliyaanzia Arusha alikofanya kazi na Radio 5 baadaye alienda Mwanza ambako alijiunga Redio Free Africa akivuma katika vipindi vya michezo, habari na mambo ya burudani.

Mwanzoni mwa miaka ya 2000 alijiunga na Radio Uhuru ambako aliendelea kufanya vipindi vya michezo na habari na mara moja moja aliendesha vipindi vya burudani. Alijiunga na ITV / Radio One mwaka 2003 alikopanua uwigo kwa kufanya vipindi vya aina mbalimbali ikiwemo vile vilivyohusu muziki wa zamani.