Mwisho wa Pancho Latino Mei 18, 1988- Oktoba 9, 2018

Muktasari:

Mtayarishaji wa muziki nchini Joshua Magawa maarufu Pancho Latino hataonekana tena nyuma ya kinanda akitengeneza midundo ya muziki katika studio za B Hitz kama ilivyozoeleka baada ya mwili wake kupumzishwa katika nyumba yake ya milele.

Historia nyingine katika muziki wa Bongo Fleva inaandikwa leo. Mtayarishaji wa muziki nchini Joshua Magawa maarufu Pancho Latino hataonekana tena nyuma ya kinanda akitengeneza midundo ya muziki katika studio za B Hitz kama ilivyozoeleka baada ya mwili wake kupumzishwa katika nyumba yake ya milele.

Pancho Latino aliyejizoea umaarufu baada ya kutengeneza nyimbo kama Dar es Salaam Stand Up wa Chid Benz, Closer wa Vannesa Mdee, Baadaye Sana wa Mabeste na Amore wa Baby Madaha safari yake hapa duniani inafikia tamati.

Mmoja wa marafiki zake aliyejitambulisha kwa jina moja la Amani anasema alikuwa na marehemu mapema wiki hii wakiogelea lakini alikumbwa na umauti baada ya kuzama.

Enzi za uhai wake, Pancho Latino alijizolea umaarufu kwa kutengeneza nyimbo mbalimbali ikiwemo wa Chid Benz , Dar es Salaam Stand Up, Baby Candy wa Dully Sykes, Closer wa Vanessa na nyinginezo nyingi.

Pancho aliyezaliwa Mei 18, 1988 ni mtoto wa mwisho kati ya watoto tisa katika familia ya mzee Joshua Magawa.

Kifo cha Pancho Latino

Baadhi ya mashuhuda wa kifo cha pacho walisema awali waliona mtu akiogelea lakini hawakujua kama hajiwezi.

Walisema baada ya kukaa muda kadhaa bila kuibuka kwenye maji ilibidi wamfuate na kukuta akiwa hajiwezi.

“Jamaa alikuwa amelalia tumbo huku akicheza cheza kwenye maji ya bahari, kumbe tayari alikuwa ameshazidiwa na maji na hajiwezi, kwa hiyo tulimuokoa kwa wakati ule,” alisisitiza.

Alisema baada ya hapo walimpakia katika boti haraka ili awahishwe hospitali lakini baadaye walipata taarifa kuwa mtu huyo amefariki dunia.

Mmoja wa viongozi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Nasoro Mohamed alisema kwa kuwa sio mzungumzaji, hawezi kueleza chochote kuhusu kisiwa hicho.

“Mkaongee na wakubwa wetu au wao wakiwaruhusu sisi ndio tutaweza kuzungumza nanyi. Hamtakiwi kupiga picha wala chochote huku,” alisema.

Wosia wake

Kaka wa marehemu, Aidan Magawa amesema mdogo wake katika wosia wake aliwahi kuagiza kuwa anataka msiba wake uwe wa kawaida na siyo kuzikwa kistaa kama inavyokuwa kwa wengine.

Amesema mdogo wake akiwa na watu wake wa karibu ambao ni wafanyakazi wenzake katika studio za B Hitz aliwaambia aisngependa msiba wake uwe wa kitaifa.

“Hakutaka kuzikwa kama mtu maarufu na ndio maana tutamuaga Lugalo, hii ni katika kumuenzi kwa kile alichokuwa akikisema mara kwa mara enzi za uhai wake,” amesema.

Akimzungumzia Pancho, Amani Joachim aliyekuwa akiishi naye anasema alikuwa mtu mwenye misimamo na akisema jambo analifanya basi atalifanya hata liwe gumu kiasi gani na akisema hataki hawezi kulifanya.

Pia, anasema alikuwa mtu asiyependa kuendeshwa kwa jambo lolote lile hata kama litakuwa linamuingizia fedha.

Akitolea mfano anasema ilifika baadhi ya vituo vya redio kugoma kucheza nyimbo ambazo amezitengeneza kutokana na mfumo wa watangazaji na wamiliki wa vituo hivyo kutaka kunyenyekewa lakini hakujali.