Mwitaliano aweka rekodi ya dunia Mlima Kilimanjaro

Raia wa Italia, Nico Valsesia ambaye ameweka rekodi ya dunia kwa kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia usawa wa bahari hadi kileleni kwa saa 24, akiendesha baiskeli kutoka Tanga hadi lango kuu la Umbwe la mlima huo kwa saa 14 na kufika katika lango hilo leo saa 11:00 alfajiri.​

Muktasari:

  • Mwongoza watalii wa kimataifa, Gaudence Festo amesema baada ya kufika katika lango hilo, Valsesia alipumzika kwa saa moja na kuanza kupanda mlima huo kwa kukimbia

 Raia wa Italia, Nico Valsesia amepanda Mlima Kilimanjaro na kuweka rekodi ya dunia ya kuupanda kwa saa 24 kutoka usawa wa bahari hadi kileleni urefu wa mita 5,895.

Valsesia aliondoka Tanga jana saa 6:10 mchana na kutumia saa 14 akiendesha baiskeli.

Aliwasili Lango la Umbwe la mlima huo leo (Ijumaa) saa 10:00 alfajiri.

Mwongoza watalii wa kimataifa, Gaudence Festo amesema baada ya kufika katika lango hilo, Valsesia alipumzika kwa saa moja na kuanza kupanda mlima huo kwa kukimbia.

Taarifa iliyotumwa kwa gazeti hili na Festo imesema timu ya kumsaidia mtalii huyo ilitangulia siku moja kabla hadi eneo la Barafu Camp, urefu wa mita 4,680 kutoka usawa wa bahari kwa ajili ya kumsubiri.

“Alifika Barafu Camp na kupokewa na timu yake ya uhamasishaji na kumsaidia iliyokuwa ikimsubiri, alipumzika kwa muda mfupi na kuanza tena safari hadi kilele cha Uhuru,” amesema Festo.

Timu hiyo iliwajumuisha Giovanni Storti ambaye alikuwa mwezeshaji mkuu, Dino Bonelli ambaye ni mpiga picha na Luca Bagnacavalli na Gabriele Zacchera ambao ni wasaidizi wake muhimu.

Festo amesema Valsesia amefanikiwa kuweka rekodi ya dunia kwa kupanda na kushuka mlima huo kwa saa nane kuanzia leo saa 11:00 alfajiri kutoka lango la Umbwe na alitarajiwa kushuka jioni.