Mzee wa Upako ampa tiki Lowassa

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo jijini Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’.

Muktasari:

  • “Nani! Lowassa…. jina lake kutajwa sana katika vikao vya CCM. Hiyo inaashiria kuwa ni mtu tishio. Ndiyo ni tishio,” alisema Lusekelo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
  • Lusekelo ambaye hivi karibuni, Rais John Magufuli alishiriki ibada katika kanisa lake, alimzungumzia Lowassa baada ya kuulizwa swali juu ya mtazamo wake kuhusu Mkutano Maalumu wa CCM ambao jina la mgombea huyo wa urais kupitia Chadema na Ukawa lilitajwa na makada wengi wa chama hicho tawala.

Dar es Salaam. Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo jijini Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’ amesema kitendo cha viongozi wa CCM kulitaja zaidi jina la Edward Lowassa katika Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho, ni ishara kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani ni tishio.

“Nani! Lowassa…. jina lake kutajwa sana katika vikao vya CCM. Hiyo inaashiria kuwa ni mtu tishio. Ndiyo ni tishio,” alisema Lusekelo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Lusekelo ambaye hivi karibuni, Rais John Magufuli alishiriki ibada katika kanisa lake, alimzungumzia Lowassa baada ya kuulizwa swali juu ya mtazamo wake kuhusu Mkutano Maalumu wa CCM ambao jina la mgombea huyo wa urais kupitia Chadema na Ukawa lilitajwa na makada wengi wa chama hicho tawala.

“Sizungumzi haya kwa ajili ya kujipendekeza, sihitaji ukuu wa wilaya,” Lusekelo aliwataka viongozi kukataa kuendeleza uhasama wa kisiasa na chuki kwa maelezo kuwa mwaka huu uwe maalumu kuzika tofauti hizo, kufanya kazi kulijenga Taifa na kuhubiri amani na umoja.