NCAA yaanza kutekeleza agizo la Majaliwa

Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Dk Freddy Manogi

Muktasari:

  • Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Dk Freddy Manogi alitoa taarifa hiyo katika uzinduzi wa ujenzi wa eneo la mifugo kunywa maji nje ya Kreta ya Ngorongoro na kuanza kutumia josho jipya la kuogesha mifugo ndani ya mamlaka hiyo.

Arusha. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imeanza kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ya kuipatia mifugo ya wananchi wanaoishi ndani ya mamlaka hiyo maji, chumvi na majosho ili isiingie ndani ya Kreta.

Mhifadhi Mkuu wa NCAA, Dk Freddy Manogi alitoa taarifa hiyo katika uzinduzi wa ujenzi wa eneo la mifugo kunywa maji nje ya Kreta ya Ngorongoro na kuanza kutumia josho jipya la kuogesha mifugo ndani ya mamlaka hiyo.

Dk Manongi alisema tangu Waziri Mkuu alipotoa maagizo ya kuzuia mifugo kuingia ndani ya eneo hilo, wafugaji walitii na sasa NCAA inaendelea na mikakati ya kuwapatia maji, chumvi na huduma nyingine muhimu.

Akizungumza katika uzinduzi wa miradi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Taka alisema Serikali itaendelea kuhakikisha wananchi wanaoishi ndani ya NCAA wanapata huduma muhimu.

Taka aliwapongeza NCAA kwa kuendelea kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi hiyo, kwa kuwapatia majosho na maji kwa ajili ya mifugo ambayo ndio tegemeo lao.

“Miradi hii tunataka iwepo maeneo mengi na itunzwe ili kuendelea kuwanufaika wananchi wa Ngorongoro na Taifa,” alisema

Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Wafugaji wa Ngorongoro, Edward Maura alitaka NCAA kuharakisha miradi ya kusaidia wafugaji kwani wao wametii agizo la Waziri Mkuu kutoingiza mifugo Kreta kufuata maji na chumvi.

Daktari wa Mifugo wa NCAA, Kimerei Saning’o alisema tarafa hiyo yenye zaidi ya mifugo, 200,000 inakabiliwa na magonjwa yanayotokana na kope na mbung’o.

Alisema kuzinduliwa kwa josho hilo katika Kijiji cha Mukulati juzi kutasaidia kupunguza magonjwa ya mifugo na kila mwezi wafugaji watatakiwa kuosha mifugo yao mara mbili.

Majaliwa akiwa ziarani Ngorongoro Desemba mwaka jana, aliagiza mifugo kutoingia Kreta na NCAA kuipatia huduma hizo.