NEC yaalika waangalizi uchaguzi mdogo wa ubunge, madiwani

Muktasari:

Yabainisha masharti 10 yanayopaswa kuzingatiwa

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa mwaliko kwa watazamani wa ndani katika uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani utakaofanyika Septemba 16, 2018.

NEC imealika waangalizi hao kushuhudia uchaguzi katika majimbo matatu ya Ukonga-Dar es salaam, Monduli-Arusha na Korogwe Vijijini-Tanga pamoja na kata 23 zilizo kwenye halmashauri 15 za Tanzania bara.

Taarifa ya NEC iliyotolewa leo Agosti 21,2018 na kusainiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi, Salvius Nkwera inataka waangalizi hao kuwasilisha maombi kuanzia Septemba 1-9, 2018.

Kware amesema kwa mujibu wa kifungu cha 46 (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 48 (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Madiwani), Sura ya 292, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kuendesha uchaguzi mdogo wa ubunge na madiwani.

“Kwa ajili ya kuweka uwazi katika uchaguzi huo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuzingatia Kanuni ya 18 (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015, na Kanuni ya 14 (2) ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (Uchaguzi wa Madiwani) za mwaka 2015,”

“Inapenda kualika asasi za kiraia na taasisi mbalimbali za ndani zinazotaka kuwa watazamaji wa uchaguzi katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Septemba 16 2018,” amesema Nkware na kuyataja majimbo hayo kuwa ni Monduli, Korogwe Vijijini na Ukonga.

Amesema asasi au taasisi zinapaswa kuzingatia masharti yafuatayo wakati wa kuwasilisha maombi; kuwa na anuani kamili ya asasi husika, anuani ya makazi ya ofisi ya taasisi husika ilipo, na mahali/sehemu ambapo taasisi husika inafanyia kazi.

Pia, shughuli ambazo zinafanywa na taasisi husika kwa mujibu wa hati ya usajili, kutaja sehemu ambazo asasi/taasisi inataka kufanya kazi hiyo ya utazamaji, kutaja idadi ya watu ambao asasi/taasisi itawatumia katika kazi hiyo pamoja na taarifa zao.

Masharti mengine ni; kutaja majina na namba za simu za viongozi wa taasisi husika kama yalivyoandikwa katika hati za usajili wa taasisi, ikiwa taasisi inahusisha watendaji wa kimataifa, wawili lazima wawe Watanzania, kuambatisha nakala/kivuli cha hati ya usajili wa taasisi husika na mwisho kuambatisha nakala/kivuli cha katiba ya taasisi/asasi husika.

“Taasisi zitakazopewa vibali vya kuwa watazamaji, zitapaswa kuzingatia mwongozo kwa watazamaji wa ndani na wa kimataifa ulioandaliwa na Tume kwa mujibu wa Kanuni ya 24 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za mwaka 2015, na Kanuni ya 20 ya Kanuni za Uchaguzi wa Madiwani za mwaka 2015,” amesema Nkware.