NEC yafafanua viapo mawakala wa uchaguzi

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Bw. Kailima Ramadhani 

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhan amesema vyama vya siasa vinapaswa kusoma sheria na kanuni zilizopo ili kuweka mikakati itakayovisaidia kufanikisha malengo yao na kushiriki uchaguzi kwa misingi iliyowekwa.

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imefafanua kuhusu malalamiko ya kucheleweshwa kwa fomu za kiapo za mawakala wa Chadema kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Kinondoni uliofanyika Februari 17 ikisema hakuna sheria wala kanuni inayotaka iwe hivyo.

Mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhan amesema vyama vya siasa vinapaswa kusoma sheria na kanuni zilizopo ili kuweka mikakati itakayovisaidia kufanikisha malengo yao na kushiriki uchaguzi kwa misingi iliyowekwa.

“Hakuna sheria wala kanuni yoyote ya uchaguzi wa Rais, wabunge au madiwani inayotaka mawakala wapewe nakala ya kiapo,” alisema Kailima jana kwa simu.

Alifafanua kuwa kutokana na changamoto inayojitokeza kwa wasimamizi wa kituo kuwatambua mawakala wa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi husika, NEC imeandaa utaratibu.

Alisema msimamizi wa kituo anapaswa kuwasiliana na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo husika ili ampe orodha ya wasimamizi hao ili kurahisisha utambuzi.

Kwa kuwa, mara nyingi, msimamizi wa kituo huwa hayupo wakati mawakala hawa wakiapa, Tume hutoa nakala ya kiapo na barua ya utambulisho na msimamizi wa uchaguzi hukubaliana na mawakala hawa muda wa kuzichukua.

Kuhusu madai kwamba msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kinondoni, Aaron Kagurumjuli alikiuka sheria kwa kuchelewa kutoa viapo kwa mawakala wa Chadema, Kailima alisema hakuna alichokosea.

Utaratibu unamtaka msimamizi wa kukubaliana na mawakala muda wa kuchukua nakala hizo kabla hazijatumika siku ya uchaguzi.

“Msimamizi hakuchelewesha fomu. Alikubaliana na mawakala wote zitolewe Februari 16, saa 12 jioni na ilikuwa hivyo. Wawakilishi wa vyama vyote waliokuwapo walipata nakala hizo,” alisema Kailima.

Kosa analoliona mkurugenzi huyo ni Chadema kuhitaji fomu hizo kabla ya muda huo haujafika tofauti na vyama vingine kumi na moja vilivyobaki na kukifanya kuwa pekee kilicholalamika.

“Siha walipewa fomu zao saa 12 jioni na hakuna aliyelalamika. Utaratibu ulifuatwa. Uchaguzi tarehe 17 inakuwaje unazitaka fomu saa 10 jioni ya tarehe 16, unataka kuzifanyia nini?” alihoji Kailima.

Alibainisha kwamba kutokana na wingi wa mawakala waliokuwapo, msimamizi wa uchaguzi alitoa viapo hivyo kwa wawakilishi wa mawakala wa vyama husika ambao walipaswa kuvigawa kwa wenzao mchakato ambao alisema Chadema walishiriki pia.

Kutokana na ucheleweshaji wa fomu hizo kama ilivyolalamikiwa na Chadema, wafuasi wa chama hicho wakiongozwa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe waliamua kuongozana baada ya kumaliza mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Buibui hatua ambayo ililifanya Jeshi la Polisi kuwatawanya na katika tukio hilo, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala.

Kailima alisema ucheleweshaji unaolalamikiwa haukufanywa na Kagurumjuli, bali mwakilishi wa Chadema aliyechukua viapo hivyo, “Tena kwa kusaini ‘dispatch’ lakini akakawia kuzifikisha nakala hizo kwa wenzake ambao mpaka asubuhi walipotakiwa kuzionyesha hawakuwanazo.”

Licha ya tukio hilo lililotokea siku ya kufunga kampeni, Kailima alizungumzia madai ya kuibwa kisha kurejeshwa kwa sanduku la kura katika Kituo cha Idrissa, Kata ya Magomeni.

Alisema hakuna malalamiko rasmi yaliyowasilishwa kwake ingawa siku hiyo alizungumza na katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji akitaka uchaguzi uahirishwe kutokana na jambo hilo.

Alisema, kwa kutambua matakwa ya sheria katika utekelezaji wa pendekezo la Dk Mashinji, aliona hakuna uwezekano wa kufanya hivyo na akamshauri cha kufanya akinukuu alivyomweleza.

“Kaka (kama wanavyoitana), hatuwezikuahirisha uchaguzi kwa makosa ya kituo kimoja. Mwambie wakala wenu ajaze fomu namba 14 akieleza mapungufu aliyoyaona.”

Hata hivyo, alisema hafahamu kama Chadema walifuata ushauri wake ama la na ripoti ya kituo hicho haikuwa na maelezo ya kushawishi kurudiwa kwa uchaguzi.