NEC yajipanga kupunguza malalamiko ya uchaguzi

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athumani Kihamia. Picha na Maktaba

Muktasari:

NEC imetangaza kuwa Septemba 16 utafanyika uchaguzi katika majimbo ya Monduli mkoani Arusha, Ukonga (Dar es Salaam) na Korogwe Vijijini (Tanga) na uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 21 zilizoko katika mikoa 10 ya Tanzania Bara.

Wakati kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani zikianza kesho, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema itaongeza nguvu ya utoaji elimu kwa vyama vya siasa ili kupunguza malalamiko.

NEC imetangaza kuwa Septemba 16 utafanyika uchaguzi katika majimbo ya Monduli mkoani Arusha, Ukonga (Dar es Salaam) na Korogwe Vijijini (Tanga) na uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 21 zilizoko katika mikoa 10 ya Tanzania Bara.

Uchaguzi katika majimbo hayo matatu unafanyika baada ya Mwita Waitara aliyekuwa mbunge wa Ukonga na Julius Kalanga wa Monduli, wote kuhama vyama kutoka Chadema kwenda CCM.

Waitara na Kalanga wamepitishwa na CCM kuwania ubunge kwenye majimbo yao.

Jimboni Korogwe Vijijini uchaguzi unafanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge, Stephen Ngonyani maarufu Profesa Majimarefu kilichotokea Julai 2. CCM imempitisha Timotheo Mzava kuwania ubunge.

Wagombea wa Chadema waliopitishwa kuwania ubunge ni, Asia Msangi (Ukonga), Amina Saguti (Korogwe Vijijini) na Yonas Laiser (Monduli).

Hadi jana, ACT-Wazalendo ilikuwa ikiendelea na mchakato wa kuwapata wagombea.

Uchaguzi katika kata 21 unafanyika baada ya madiwani wengi kujizulu kutoka vyama vya upinzani na kujiunga na CCM, wengi wakisema wanakwenda kuunga mkono juhudi za maendeleo za Rais John Magufuli.

Katika uchaguzi uliopita wa Agosti 12 uliohusisha Jimbo la Buyungu na udiwani kwenye kata 77, yalijitokeza malalamiko yakiwamo ya mawakala kuzuiwa kuingia kwenye vituo na fomu za wagombea kutojazwa ipasavyo.

Kwa sababu hizo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athumani Kihamia alisema juzi kuwa wamejipanga kupunguza malalamiko na kwamba nguvu kubwa itaelekezwa katika utoaji elimu.

“Tutaongeza nguvu eneo la elimu hususan kwa vyama vya siasa ili kupunguza malalamiko yanayojitokeza kwa kuwa huwezi kuyamaliza,” alisema Dk Kihamia.

Alisema wamebaini baadhi ya malalamiko yanatokana na elimu ikiwamo suala la mawakala, ujazaji wa fomu za wagombea akitolea mfano wa dereva ambaye anaweza kusababisha ajali kwa magari mengine ambayo hayakuwa na kosa.

“Ni ngumu kuondoa malalamiko yote, ni kama mchezo wa mpira wa miguu, mtu anapofungwa atatoa malalamiko iwe kwa mwamuzi au kwa nani, kwa hiyo tunajitahidi kuongeza elimu ili kupunguza malalamiko,” alisema Dk Kihamia.