Zuma afikishwa ukingoni

Muktasari:

Afrika Kusini inapitia kipindi cha sintofahamu na wasiwasi kutokana na suala hili ambalo “linamomonyoa matarajio mapya na imani miongoni mwa wananchi wa Afrika Kusini tangu mkutano wa 54 wa kitaifa wa ANC

Pretoria, Afrika Kusini. Rais Jacob Zuma anaweza kutumia kila hila kujichelewesha kujiuzulu lakini ‘kifo chake kisiasa’ kimetiwa saini Jumanne baada ya chama chake cha ANC kutangaza rasmi kuwa kimemwandikia barua ya kumtaka ang’atuke.

Katika mkutano wa waandishi wa habari Jumanne mchana kwenye makao makuu ya Luthuli, Katibu Mkuu wa ANC, Ace Magashule alithibitisha kwamba maofisa wa chama walimpelekea Zuma uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa kumtaka ajiuzulu.

"NEC imepokea ripoti kutoka kwa maofisa wa taifa kuhusu kikao chao na rais. NEC inajua kwamba maofisa wamekubaliana naye kimsingi kwamba ajiuzulu. Rais alipendekeza kuwa apewe muda wa miezi sita kubaki ofisini,” alisema Magashule.

Hata hivyo, katika taarifa yake NEC imesema inaelewa kwamba Afrika Kusini inapitia kipindi cha sintofahamu na wasiwasi kutokana na suala hili ambalo “linamomonyoa matarajio mapya na imani miongoni mwa wananchi wa Afrika Kusini tangu mkutano wa 54 wa kitaifa wa ANC".

NEC iliamua kwa mara nyingine kuzungumza na Zuma juu ya haja ya kutatua suala hili kwa haraka, lakini hakukubali likamilike katika muda mfupi. Hali hiyo ndiyo ilisababisha uamuzi wa kumtaka ajiuzulu.

"Uamuzi wa NEC kumtaka mwajiriwa wake ajiuzulu ulichukuliwa baada ya kumalizika njia zote za majadiliano kuhusu madhara kwa nchi kwa yeye kujiuzulu katika uongozi wa nchi, ANC na serikali,” alisema Magashule.

Alisema chama kinamtaka Rais wa ANC, Cyril Ramaphosa kuchukua majukumu ya uongozi wa nchi.

"Uamuzi wa NEC unatoa hakikisho kwa wananchi wa Afrika Kusini katika kipindi ambacho kuna changamoto za kiuchumi na kijamii ambazo zinahitaji ufumbuzi wa haraka wa jamii,” taarifa ya NEC iliongeza.

 

Saa 13 za mkutano

Halmashauri Kuu ilifanya mkutano wa saa 13 mfululizo huko Irene nje kidogo ya Pretoria. Mkutano huo ulioitishwa kwa dharura ulianza saa 8:00 Jumatatu mchana na kumalizika saa 9:00 usiku kuamkia Jumanne.

Saa 5:00 usiku NEC iliamuru kuwatuma Ramaphosa na Katibu mkuu Ace Magashule kwenda nyumbani kwa Zuma kwenye makazi yake Mahlamba Ndlofu mjini Pretoria kumpa hati ya kujiuzulu au kukubali kufukuzwa na chama.

Kikao kati ya wajumbe wawili hao na Zuma kilidumu chini ya saa moja ambapo mkuu huyo wa nchi alikataa kutii.

Ramaphosa na Magashule walirudi kwenye mkutano wa NEC na kutoa mrejesho saa 6:00 usiku. Ukumbi ulikuwa umefungwa wakati ambapo wale wawili waliondoka kwenda kukutana na Zuma.

Vyanzo kutoka ndani ya NEC viliarifu shirika la News24 kwamba wakati wa kikao cha watatu hao Zuma aliwauliza wajumbe waliotumwa: "Kitu gani kibaya nimefanya".

"Zuma aliwajibu Ramaphosa na Magashule kuwa atawajibu hadharani chama kitakapokuwa kimeamua kumwita," kilisema chanzo.

Jumanne mchana ANC ilizungumza na vyombo vya habari juu ya matokeo ya mkutano wa NEC saa 6:00 Jumanne mchana.

 

Muda anaoomba

Zuma inasemekana anataka kuendelea kubaki kwenye majengo ya serikali yaitwayo Union Buildings kwa miezi kati ya mitatu na sita ili aweze kushiriki matukio mawili. Hata hivyo, NEC ilikataa masharti yake.

Vyanzo vilisisitiza kuwa Zuma alitaka kubaki kama mkuu wa serikali hadi wakati mkutano wa kilele wa nchi nne za Brics utakapofanyika na alitaka kuhudhuria mkutano mwingine wa Umoja wa Afrika.

Mkutano wa Brics umepangwa kufanyika Julai mjini Sandton ikiwa na maana Zuma atakuwa madarakani kwa miezi mitano zaidi. Zuma aliongoza Afrika Kusini kuingia kwenye umoja wa kiuchumi wa Brazil, Russia, India na China.

 

Programu za Bunge

Shirika la habari la TimesLIVE limeripoti Jumanne kwamba Magashule na naibu wake Jessie Duarte walipewa jukumu la kumpelekea Zuma barua asubuhi ya kumfahamisha uamuzi wa NEC wa kumtaka ajiuzulu.

Hatua hiyo imeathiri hata programu za Bunge. Hotuba kwa taifa ambayo ilikuwa itolewe Alhamisi iliyopita iliahirishwa.

Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) kinachoongozwa na Julius Malema kimemwomba Spika wa Bunge, Baleka Mbete kurudisha nyuma tarehe ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Rais Zuma.

Kadhalika, wabunge wa ANC wamepewa taarifa ya kufanyika kikao cha wabunge Jumatano.

"Kutokana na hali hii‚ mnadhimu mkuu ameomba kwamba kikao cha wanadhimu wakuu (kinajumuisha na wa upinzani) ambacho kwa kawaida huwa kinafanyika saa 4:00 asubuhi kifanyike saa 2:00 asubuhi,” alisema Nonceba Mhlauli‚ ambaye ni msemaji wa ofisi ya mnadhimu mkuu wa ANC, Jackson Mthembu.