Vyama kuwasilisha majina ya mawakala mwisho kesho

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima

Muktasari:

  • Uchaguzi huo utafanyika Februari 17, 2018.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kesho, Februari 10, 2018 ndio mwisho kwa vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni na Siha na udiwani kwenye kata tisa kuwasilisha majina ya mawakala wao.

Taarifa ya NEC, iliyotolewa leo Februari 10, 2018, inamnukuu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhan Kailima akisema hatua hiyo ni kwa mujibu wa kifungu namba 57 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Sura ya 343) na kifungu namba 58 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa (Sura ya 292) ambazo zinabainisha majina ya mawakala  wa vyama vya siasa yanatakiwa kuwasilishwa kwa msimamizi wa uchaguzi siku saba kabla ya uchaguzi.

“Uchaguzi utafanyika  Februari 17, 2018, hivyo siku saba kabla ya uchaguzi ni kesho Februari 10, hivyo nivisihi vyama vyote vya siasa vilivyosimamisha wagombea, kama vikitaka kuweka mawakala  kwenye uchaguzi huo, vipeleke orodha yao yaani utambulisho wa barua na kesho Jumamosi ndio siku ya mwisho,” amesema Kailima.

“Ikifika Februari 11 yaani Jumapili wasimamizi wa uchaguzi hawataruhusiwa kupokea orodha ya mawakala wa vyama vya siasa,” amesisitiza Kailima na kuongeza orodha hiyo ya mawakala kwa mujibu wa sheria iwe inaonyesha jina la wakala, anuani yake na kituo ambacho chama kimependekeza wakala aende kusimamia.

Amesema mawakala hao wa vyama vya siasa wanatakiwa kula kiapo cha kutunza siri kwenye fomu namba 6 siku saba kabla ya uchaguzi, hivyo kesho mawakala wote wanatakiwa wale kiapo hicho na wasipofanya hivyo kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi hawataruhusiwa kuwa mawakala wa vyama vya siasa katika uchaguzi huo mdogo.

Kailima amesema mawakala hao wanatakiwa wawe na barua ya utambulisho kutoka katika chama chake kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi na pia wawe na barua ya utambulisho kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi kwenda kwa msimamizi wa kituo.

“Ili wakala akamilike lazima awe na barua kutoka kwenye chama chake, ale kiapo na awe na barua ya utambulisho kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi kwenda kwa msimamizi wa kituo, hivyo navishauri vyama vya siasa vizingatie hili,” amesema Kailima.

Pia mkurugenzi wa uchaguzi amefafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu namba 47 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi (Sura ya 343) na 49 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa (Sura ya 292), siku nane kabla ya uchaguzi, wasimamizi wa uchaguzi wanatakiwa watoe tangazo la uchaguzi, hivyo akawataka wasimamizi wa vituo kuhakikisha wanaweka matangazo hayo Februari 9, 2018.

 “Tangazo hilo liwe linafafanua siku na muda wa kupiga kura, orodha ya wapiga kura na orodha ya mfano ya kupigia kura,” amesema Kailima.

Ametoa wito kwa wapiga kura waende wakaangalie jinsi majina yalivyopangwa kwenye orodha hiyo katika kila kituo ili wawezeshwe kupiga kura vizuri siku ya Februari 17.

Kailima amevitaka vyama vya siasa viwahamize wafuasi wao waende kuangalia orodha ya majina katika vituo vyao vya kupigia kura na wananchi wa kata za Kigogo, Kijitonyama na Mwananyamala ambao vituo vyao vimehamishwa waende ambako vituo vimehamishiwa.

Katika Kata ya Kijitonyama vituo 6 vilivyokuwa katika shule ya Sekondari Kenton vimehamia shule ya Msingi Mapambano na vituo 5 vilivyokuwa nje ya Ofisi ya serikali ya Mtaa wa Bwawani vimehamishiwa mbele ya ofisi hiyo.

Vituo sita vilivyokuwa nje ya soko la Makumbusho vimehamia ndani ya Ofisi ya Meneja wa Soko hilo na vituo 5 vilivyokuwa katika Ofisi ya Serikali za mitaa Kijitonyama vimehamishiwa katika Shule ya Msingi Kijitonyama.

Katika Kata ya Kigogo vituo 16 vimehamishwa, vituo vitano vilivyokuwa eneo la Kiwenge kwenye Msikiti wa Shiha vimehamia Uwanja wa People na Vituo 6 vilivyokuwa kwenye Zahanati ya Kigogo vimehamishiwa Shule ya Kigogo na vituo vitano vilivyokuwa katika ofisi ya Serikali ya Mtaa Mkwajuni vimehamishiwa Shule ya Sekondari Kigogo.

Amesema Kata ya Mwananyamala ina vituo vya kupigia kura 65 na wapiga kura 27,589 na vituo vinane (8) vilivyokuwa Shule ya Sekondari Kambangwa mtaa wa Msisiri A vimehamishwa. Kati ya hivyo 6 vimehamishiwa katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa ya Msolomi na viwili kuhamishiwa Uwanja wa Kwakopa.