NEC yawalima barua Chadema

Mkurugenzi wa Opareshi na Mafunzo Chadema, Benson Kigaila akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Amesisitiza wataendelea kupigania haki ya wagombea wa chama hicho na wanakwenda kushinda kwenye uchaguzi huo.


Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeiandikia barua Chadema ikitaka utambulisho wa mawakala watakaosimamia uchaguzi wa marudio wa jimbo la Buyungu na Kata 77 Agosti 12, 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 18, 2018 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Operesheni na Mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila amesema barua hiyo inawaelekeza wakala atatambulishwa kwa msimamizi wa uchaguzi kwa barua ya chama, picha mbili za pasapoti na kitambulisho chochote chenye picha.

Hata hivyo, Kigaila amekosoa uamuzi huo wa Tume kwa madai hawajapewa mwongozo wowote wa mawakala siku ya kupiga kura, jambo linaloweza kusababisha sintofahamu kama ilivyokuwa kwenye uchaguzi wa jimbo la Kinondoni.

"Kwenye uchaguzi uliopita wa Kinondoni mawakala wetu waliambiwa hawana utambulisho wowote kutoka Tume, jana wametuandikia barua wanatoa masharti lakini hawasemi siku ya uchaguzi itakuwaje, mawakala watatambuliwa vipi," amesema Kigaila.

Kigaila amesema Tume hiyo haijayafanyia kazi malalamiko ya Chadema licha ya kuandikiwa barua na Katibu Mkuu wake, Dk Vincent Mashinji kukutana na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Dk Athumani Kihamia.

Amesisitiza wataendelea kupigania haki ya wagombea wa chama hicho na wanakwenda kushinda kwenye uchaguzi huo.

"Mkurugenzi ametuambia ili kuepusha makosa yaliyofanyika kwenye uchaguzi wa Kinondoni mawakala waje na vitambulisho. Kumbe wanatambua Uchaguzi wa Kinondoni ulikuwa na kasoro lakini hawajamchukulia hatua zozote msimamizi wa uchaguzi wa Kinondoni kwa kuharibu uchaguzi," amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi amewataka polisi kufanya kazi zao badala ya kuingilia uchaguzi kwa kuwakamata wagombea wa Chadema.

"Kuna kata 18 ambazo wagombea wa Chadema wameenguliwa. Mpaka sasa kuna maeneo watu wetu wamekataliwa rufaa zao, kwa mfano Rombo. Tumeandika malalamiko yetu kwa Tume," amesema Munisi.