NMB yafanya kufuru Nyanda za Juu

Muktasari:

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Tawi la NMB Uyole lililopo mkoani Mbeya, Meneja wa Kanda ya Nyanda za juu - Badru Iddy amesema kuwa lengo la benki hiyo ni kusogeza huduma zaidi kwa wananchi ili kuwa karibu na wateja wake.

Mbeya. Benki ya NMB Imefungua matawi saba kwa mpigo katika mikoa sita katika juhudi za kujiimarisha zaidi na kuwa karibu na wateja wake wa kanda ya nyanda za juu.

Matawi hayo yamefunguliwa katika mikoa ya Njombe, Mbeya, Songwe, Rukwa na Katavi. Matawi ambayo yamefunguliwa na yanatoa huduma kwa jamii ni pamoja na NMB  Kasumulu, NMB Uyole, NMB Mkwajuni, NMB Wanging’ombe, NMB Laela na NMB Kalambo lililopo Mlele.

Idadi hiyo ya matawi mapya inafanya jumla ya matawi ya NMB 31 katika Kanda ya Nyanda za Juu huku yakifikia matawi ya NMB 207 nchi nzima.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Tawi la NMB Uyole lililopo mkoani Mbeya, Meneja wa Kanda ya Nyanda za juu - Badru Iddy amesema kuwa lengo la benki hiyo ni kusogeza huduma zaidi kwa wananchi ili kuwa karibu na wateja wake.

“Kuzinduliwa  kwa tawi hili la NMB Uyole mahali hapa kunafuatia mahitaji ya muda mrefu ya wateja wetu wa Uyole kupata tawi la NMB lenye nafasi ya kutosha. Aidha  eneo hili ni karibu zaidi na wafanyabiashara wengi ambao ni wateja wetu wakubwa na wananchi kwa ujumla .Tawi hili  kama yalivyo matawi yetu mengine nchini linatoa huduma zote za kibenki zitolewazo na benki yetu," alisema Badru.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tawi la Uyole, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alisema kuwa wananchi wanapaswa kufungua akaunti katika benki hiyo na kuitumia kwa kuwa Serikali ina hisa ya asilimia 32 katika benki hiyo.

“Hapa tuelewane, Serikali na benki ya NMB ni sawa na mapacha kwa kuwa kila mahala ambapo Serikali imepeleka huduma zake za kijamii benki hiyo hufuatia kwa kuweka huduma za kifedha ili kuwahudumia wananchi wa eneo husika,” alisema Makalla.

Mkoani Songwe Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Samwel Jeremiah ambaye  alimwakilisha mkuu wa mkoa huo, Chiku Galawa kwenye uzinduzi wa tawi la NMB Mkwajuni,  aliwataka wananchi  kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na hivyo kutumia fursa zinazotokana na benki ya NMB kukuza uchumi wao na mwisho kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.