NMB yahukumiwa Sh12 milioni kwa kukiuka taratibu za kikandarasi

Muktasari:

Mkurugenzi wa kampuni hiyo ya ukandarasi, Japhet Sanga ametakiwa kulipa Sh3 milioni kutokana na kujipatia kazi kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria.


Mbeya. Benki ya NMB imehukumiwa kulipa jumla ya Sh12 milioni baada ya kuipa kazi kampuni ya Kalongo’s General Supply ambayo haijasajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).

Wakati benki hiyo ikihukumiwa kutoa kiasi hicho kutokana na makosa matatu iliyothibitika kuyatenda, mkurugenzi wa kampuni hiyo ya ukandarasi, Japhet Sanga ametakiwa kulipa Sh3 milioni kutokana na kujipatia kazi kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria.

Akisoma hukumu hiyo leo, Julai 17, hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama hiyo, Michael Mteite amesema NMB imekutwa na makosa matatu likiwamo la kumpa kazi mkandarasi ambaye hajasajiliwa na CRB.

Makosa mengine ni kukaidi tahadhari iliyotolewa na CRB na kutotii agizo lililoitaka benki hiyo kutoendelea na kampuni hiyo  na kuweka mifumo ya kuzuia na kuzima moto kwenye matawi ya benki hiyo yaliyopo Nyanda za Juu Kusini.

“NMB ina hatia kwa makosa yote matatu na itatakiwa kulipa faini ya Sh4 milioni kwa kila kosa ndani ya siku 30 na ikishindwa kufanya hivyo mahakama itaamuru meneja wake kwenda jela miaka mitatu kwa kila kosa na adhabu hiyo itatumikiwa kwa wakati mmoja,” alisema Hakimu huyo.

Kifungo cha miaka mitatu jela pia kitamuhusu Sanga endapo atashindwa kulipa faini aliyopewa na mahakama hiyo.