NMB yakabidhi Serikali gawio la Sh10 bilioni

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akipokea mfano wa hundi ya Shilingi Bilioni 10.17 Ofisi ya Wizara ya Fedha mjini Dododma jana kutoka kwa Mkurungenzi wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker (wa pili kulia) ikiwa ni gawio la Serikali. Katikakati ni Msajili wa Hazina Nchini, Athuman Mbutuka. Picha na Mpiga picha Maalum

Muktasari:

  • Fedha hizo ni sehemu ya jumla ya Sh32 bilioni ambazo ziliidhinishwa na mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa wa benki hiyo, uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Dodoma. Benki ya NMB imekabidhi gawio la Sh10.17 bilioni kwa Serikali kutokana na faida iliyopatikana mwaka 2017.

Fedha hizo ni sehemu ya jumla ya Sh32 bilioni ambazo ziliidhinishwa na mkutano mkuu wa mwaka wa wanahisa wa benki hiyo, uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, wanahisa waliidhinisha kutolewa gawio la jumla ya Sh32 bilioni kutokana na NMB kupata faida ya baada ya kodi ya Sh93.3 bilioni kwa mwaka 2017.

Mkurugenzi mtendaji wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker akizungumza kabla ya kukabidhi mfano wa hundi ya Sh10.17 bilioni kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, alisema benki imejikita kuhakikisha Watanzania wengi zaidi hasa wakulima wanapata huduma za benki popote walipo.

Bussemaker alisema mbali na gawio hilo, NMB ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa nchini ikiwa imelipa Sh127 bilioni kama kodi mbalimbali za Serikali kwa mwaka 2017 pekee.

“Pamoja na hayo, tunatenga asilimia moja ya faida yetu na kuipeleka katika kuboresha huduma za jamii. Mwaka jana pekee tulinunua na kusambaza madawati 6,000,” alisema Bussemaker.

Takwimu zinaonyesha ni asilimia 17 tu ya Watanzania watu wazima ambao wanamiliki akaunti katika benki za biashara.

Kutokana na hali hiyo, NMB imeongeza juhudi za kuhamasisha wakulima wafungue akaunti. Mwaka jana akaunti 300,000 zilifunguliwa na kuiwezesha benki kuongeza idadi ya wateja kufikia milioni 2.7.

Akizungumza kabla ya kupokea mfano wa hundi, Dk Mpango aliishukuru NMB kwa kuendelea kupata faida licha ya kukiri kuwa mwaka jana ulikuwa na changamoto nyingi kwa sekta ya fedha.

“Mwaka 2017 haukuwa mzuri kwa sekta ya fedha ila nina furaha kujua kwamba NMB iliweza kupata faida na leo wanatoa gawio kwa Watanzania maskini. Hii inadhihirisha ukweli kwamba NMB ina uongozi na usimamizi madhubuti katika utoaji wa huduma zake,” alisema Dk Mpango.

Aliuhakikishia uongozi wa NMB kuwa gawio hilo litatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Waziri huyo pia alitoa rai kwa kampuni nyingine ambazo kuna hisa za Serikali kuiga mfano wa benki hiyo na kuanza kutoa gawio.