NYANZA: Bodaboda wageuka janga kwa wanafunzi wa kike

Muktasari:

USULI
“Utafiti uliofanywa hivi karibuni na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa) unaonyesha katika kipindi cha mwaka 2012/2013 matukio 228 ya mimba  na 42 ya  ndoa za utotoni  yaliripotiwa
Hata hivyo, mimba na ndoa za utotoni  zimetajwa kuwa ni miongoni mwa vikwazo vinavyowapata watoto wa kike  wengi Tanzania Bara na Visiwani kutimiza malengo yao ya baadaye.

Wakati  Tanzania Zanzibar  hali ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ikionekana zaidi katika Mkoa wa Kusini Pemba na Wilaya ya Kati Unguja, upande wa Tanzania Bara  maeneo yenye ukatili dhidi ya wanawake pamoja na mimba za utotoni yanaonekana katika wilaya za  Kahama, Tarime, Sengerema, Newala, Mbulu, Bunda, Nkasi, Babati, Chunya, Dodoma, Bariadi, Busega na Singida Vijijini, hali hiyo imejitokeza pia katika Wilaya ya Rorya mkoani Mara kama makala hii inavyoeleza.

Rorya. Mbinu ya kuwapa lifti wakati wa kwenda au kurudi shule ndiyo chambo inayotumiwa na waendesha bodaboda kuwanasa kimapenzi wanafunzi wa kike.

“Fadhila ya lifti inaangamiza watoto wetu wanaoishi mbali na maeneo ya shule,” anasema Mwalimu Ochola.

Hata hivyo, siyo waendesha bodaboda wote wanashiriki vitendo vya ngono na wanafunzi kama ambavyo Nicolas Odemba anayefanya biashara ya kusafirisha abiria kwa kutumia pikipiki anavyosema wakati wa mahojiano maalumu yaliyofanyika katika mji mdogo wa Shirati anakofanyia shughuli zake.

 “Nachukizwa na tabia ya baadhi yetu kuwarubuni na kujihusisha kimapenzi na wanafunzi wa kike ambao huishia kupata ujauzito.

Kwa umri wangu wa miaka 45, watoto hawa wana umri sawa na wanangu,” anasema Odemba na kuongeza:

“Tayari tumeunda kamati maalumu ya kukabiliana na kadhia hii inayotuchafulia jina katika jamii.”

Anasema licha ya lifti, waendesha bodaboda wenye tabia ya kuwarubuni wanafunzi na kusababisha kundi hilo ‘kubatizwa’ jina la ‘mtambo wa kufyatua mimba’ kwa wanafunzi hutumia pia kuwahadaa kwa kuwapa zawadi ya fedha taslimu kati ya Sh1, 000 hadi 2, 000.

Shughuli za uchumi na umasikini wa kipato

Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Chacha anataja umasikini wa kipato na mwamko mdogo wa kielimu ni miongoni mwa jamii wilayani mwake kuwa ni sababu kuu ya tatizo la mimba shuleni.

“Baadhi ya wazazi hawamudu kuwapatia mahitaji muhimu watoto wao wa kike ikiwamo fedha za kununulia taulo za kike (pedi), nguo na hata chakula wawapo shuleni; hali inayowalazimisha wanafunzi kunasa kwenye mitego ya walaghai wanaowarubuni hata kwa Sh500,” anasema.

Akizungumzia wanafunzi wa kiume, Mkuu huyo wa wilaya anataja ushiriki wao kwenye shughuli za kiuchumi ikiwamo uvuvi katika Ziwa Victoria, ufugaji na biashara ya bodaboda kuwa ni kati ya sababu kuu za kuacha masomo.

“Uwapo wa Ziwa Victoria ni neema, lakini wakati mwingine unatumika vibaya kwa kusababisha watoto wetu kukimbilia uvuvi badala ya kusoma,” anasema Chacha.

Graca Machel kuleta ahueni

Mpango wa kuwarejesha shuleni wanafunzo 20,000 waliokatisha masomo mkoani Mara uliotangazwa na taasisi ya mjane wa Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Graca Machel huenda ukaleta mwanga mpya mkoani Mara wenye wilaya sita, Rorya ikiwamo.

Mradi huo wa zaidi ya Sh8 bilioni ambazo nusu yake zitatolewa na taasisi ya Graca Machel na nyingine Serikali, unasimamiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma, Serikali, taasisi ya Equip Tanzania na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na utetezi wa haki za watoto, utawarejesha shuleni wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu ya kupata ujauzito, utoro na ndoa za utotoni.

Wazazi, mahari kikwazo hatua dhidi ya wahusika

Kisheria, kumpa ujauzito mwanafunzi ni kosa la jinai linalostahili muhusika kufungwa gerezani kifungo cha hadi miaka 30 pale anapobainika kufanya hivyo, lakini hali ni tofauti wilayani Rorya ambako wanaowapa mimba wanafunzi huachwa wakipeta mitaani baada ya kulipa mahari.

“Wazazi ni kikwazo cha udhibiti wa mimba shuleni kwa sababu huwatorosha watoto wao kukwepa hatua za kisheria dhidi ya wahusika baada ya kupokea mahari,” anasema Mratibu wa Elimu Kata ya Mkoma, Bernard Oloo.

Anasema kabla ya kuwatorosha watoto wao, wazazi hao hutumia barua au hati zinazothibitisha ujauzito wa wanafunzi hao kuwatishia waliowapa ujauzito ambao kwa kuogopa kifungo, hutoa mahari na malipo mengine kama fidia na kifunga mdomo kwa wazazi.

“Katika jamii yetu, mahari ni moja ya vyanzo vya mapato kwa wazazi wenye watoto wa kike. Hiki ni kikwazo cha mapambano dhidi ya wanaowapa mimba wanafunzi na Serikali inapaswa kudhibiti tabia hii kwa nguvu zote,” anasema Oloo.

Kwa nini wazazi wanachukua mahari mambo yaishe?

“Kwa nini nisichukue mahari wakati hata nikimuacha muhusika hatachukuliwa hatua kwa sababu mtoto aliyepewa ujauzito anaweza kumficha ili kumlinda kutokana na mapenzi kati yao?” anahoji Antony Kagose.

Akijibu swali la kwa nini wazazi wanakwamisha hatua za kisheria dhidi ya wanaowapa ujauzito watoto wao, Kagose ambaye ni mkazi wa Ingri Juu yaliko makao Makuu ya Wilaya ya Rorya anataja umasikini wa kipato na vitendo vya rushwa kuwa miongoni mwa sababu.

“Fikiria mzazi kauza mifugo yake yote kumsomesha mtoto tangu kidato cha kwanza hadi cha nne, halafu anafukuzwa shule kwa kupata ujauzito. Lazima achukue mahari kufidia hasara kutekeleza usemi wa heri nusu shari kuliko shari kamili,” anase a Kagose na kuongeza:

“Wakati mwingine mzazi anaamua kuchukua hatua za kisheria, lakini mhusika anaachiwa huru na vyombo vya dola na sheria kwa madai ya kukosekana ushahidi.”

Mzazi huyo anataja rushwa miongoni mwa watendaji katika vyombo vya uamuzi kuwa ni chanzo nyingine kwa wanaowapa ujauzito wanafunzi kutochukuliwa hatua za kisheria.

Nini kifanyike kukabiliana na mimba shuleni?

“Kwanza wazazi wawe watu wa kwanza kuchukua hatua dhidi ya wanaowapa ujauzito watoto wao kwa sababu wahenga walisema kilio huanza kwa mfiwa,” anasema Oloo na kuongeza:

“Wazazi pia wahakikishe wanawapa mahitaji na huduma zote muhimu watoto wao ili kuwaepusha na vishawishi vinavyochochewa na uduni wa maisha.”

Itaendelea kesho.