Nabii Afrika Kusini amtabiria ugonjwa kiongozi wa upinzani

Kiongozi wa Kanisa la Enlightened Christian Gathering (ECG) la Afrika Kusini, Nabii Shepher Bushiri

Muktasari:

Nabii Bushiri pia amesema mwaka 2018 utakuwa mgumu kwa Tanzania kuliko wakati mwingine wowote, akishauri wananchi wafanye maombi kuiepusha nchi na hali hiyo.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa la Enlightened Christian Gathering (ECG) la Afrika Kusini, Nabii Shepher Bushiri amemtabiria ugonjwa hatari kiongozi wa upinzani wa Tanzania, akisema maombi pekee na imani yake ndio vitamnusuru asitokewe na “kitu kibaya”.

Nabii Bushiri pia amesema mwaka 2018 utakuwa mgumu kwa Tanzania kuliko wakati mwingine wowote, akishauri wananchi wafanye maombi kuiepusha nchi na hali hiyo.

Bushiri alisema hayo wakati wa ibada ya Sikukuu ya Pasaka iliyofanyika katika kanisa lake nchini Afrika Kusini na kurushwa moja kwa moja katika mitandao ya kijamii.

“Tanzania itapata shida ambayo haijawahi kuiona. Sisi kama kanisa, ni jukumu letu kuyaombea mataifa kwa sababu tumeitwa kwa ajili ya mataifa,” alisema Nabii Bushiri akiwa ameshika bendera ya Taifa ya Tanzania mkononi na shingoni akiwa amejifunga skafu yenye rangi za bendera hiyo.

“Tunaiombea Tanzania katika mwaka 2018, huruma za Mungu ziwe juu ya Tanzania kwa mwaka 2018. Tunaomba katika jina la Yesu. Tunaomba ulinzi.”

Wakati akiendelea na maombi hayo katika kanisa lililojaa waumini walioshika bendera za nchi zao, Bushiri aligeuzia maombi kwa ajili ya kiongozi huyo wa upinzani Tanzania.

“Tunamuombea kiongozi wa upinzani, kiongozi wa upinzani. Naona tatizo linaibuka kwenye ini lake. Lakini tunaomba huruma (ya Mungu) nazungumza kijasiri kadri ninavyoweza, kwa sababu najua (hili) linatoka kwa Bwana,” alisema nabii huyo. “Narudia hili. Nililizungumza miezi kadhaa iliyopita, (lakini) narudia kuhusu huyu mtu. Muda mfupi ujao ataanza kuzizima kama mtu anayesikia baridi. Lakini ni shambulizi hatari ambalo linahitaji maombi. Bila hivyo, kitu kibaya kitamtokea.

“Lakini mimi na wewe tunaweza kuzuia kama hata yeye ana imani. Lakini tatizo ni kwamba sioni imani kwake. Tunamuombea na tunaomba ulinzi. Inaweza isitokee sasa, lakini tunaomba ulinzi wa maisha yake.”

Nabii Bushiri ni mzaliwa wa Malawi, lakini anafanya huduma zake na biashara nchini Afrika Kusini ambako amejizolea waumini kutoka mataifa mbalimbali.

Bushiri aliwahi kutabiri kutokea kwa tetemeko la ardhi nchini Tanzania wakati alipotembelea Dar es Salaam Julai mwaka jana. “Nakumbuka mwezi uliopita, Mungu alinituma Tanzania kwenda kuzuia mauti. Nilikuwa nasali saa 1:00 asubuhi na nusu yake ikageuka kuwa damu,” alisema Bushiri katika mahubiri yake ya Julai 14, 2016 jijini Dar es Salaam.

“Nilimuuliza Mungu, nini maana yake. Na Mungu akaniambia ‘siku ya damu inakuja’. Nikasema hilo ni nini. Niliona watu wakifanya mambo yao na ghafla nikaona damu ardhini. Na Mungu akaniambia ‘iombee Tanzania’.

“Nilipokuwa nikiomba, nikaanza kutetemeka. Mwili wangu ulikuwa ukitetemeka. Na nikamuuliza Mungu, mtetemeko huu ni wa nini? Na Mungu akaniambia ‘hili ni tetemeko la ardhi. Si Dar es Salaam. Kutakuwa na tetemeko sehemu nyingine ya nchi.”

Katika ibada hiyo, Nabii Bushiri aliwataka waumini wake waiombee Tanzania kuiepusha na janga hilo.