Dk Tulia akabidhi jengo la upasuaji Mbeya

Muktasari:

Ukarabati wa jengo hilo uliofanywa na taasisi ya naibu spika huyo ya Tulia Trust, umegharibu Sh40milioni.

 Naibu Spika wa Bunge,  Dk Tulia Ackson amekabidhi mradi wa  jengo la upasuaji  katika Kituo cha Afya Ruanda cha jijini hapa  kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,  Amos Makalla.

Ukarabati wa jengo hilo uliofanywa na taasisi ya naibu spika huyo ya Tulia Trust, umegharibu Sh40milioni.

Dk Tulia amekabidhi jengo hilo leo Jumatano Machi 7, 2018 katika ziara yake mkoani hapa sambamba na kukagua  ukarabati wa mradi  huo na kuzungumza na wananchi na wagonjwa waliofika kupata matibabu katika  kituo hicho.
Amesema katika kuunga mkono jitihada za Serikali, taasisi yake imelenga kuboresha huduma  muhimu za  afya za  wajawazito na watoto  katika vituo vya afya na zahanati.
"Mkuu wa mkoa (Makalla) nakupongeza kwa jitihada zako mpaka kufikia hatua za mwisho za kusimamia mradi huu   sasa ninaomba changamoto za  mahitaji madogo  yaliyopo  yafanyiwe kazi  ili huduma za upasuaji zianze kutolewa," amesema.
Kwa upande wake Makalla amesema Serikali imetoa Sh700  milioni kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kisasa katika Kituo cha Afya Ruanda pamoja na vifaa tiba.
"Naibu Spika ukarabati wa chumba cha upasuaji umekuwa chachu kwa Serikali na sasa imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kisasa katika kituo hiki kwa kweli unatupa moyo sana kama viongozi wa Mkoa," amesema.
Pia, ameagiza halmashauri ya jiji kupitia mapato yake ya ndani kutoa fedha kwa ajili ya kumalizia baadhi ya mahitaji katika chumba cha upasuaji ili kianze kutoa huduma kwa wananchi
"Natoa wiki mbili ukarabati huu uwe umekamilika na huduma zianze kutolewa mapema iwezekanavyo," amesema.

Mganga mfawidhi  wa kituo hicho, Elioth Sanga amesema  wametenga Sh55 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upasuaji.