Naibu Waziri akagua daraja la Kelema Kondoa

Kondoa. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Edwin Ngonyani, amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa daraja la Kelema lenye urefu wa mita 220 linalounganisha wilaya ya Chemba na Kondoa mkoani Dodoma.

Akizungumza leo mkoani Dodoma, mara baada ya kukagua daraja hilo lililopo katika barabara ya Mayamaya-Mela KM 99.35, Ngonyani  amesema kuwa kukamilika kwa daraja hilo na  barabara za maingilio katika daraja hilo kutarahisisha  huduma ya usafiri kwa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani ya  Manyara na Arusha.

"Daraja hili na barabara zake ni kiungo muhimu kati ya mkoa huu na mikoa  ya Manyara na Arusha  na pia inaunganisha  nchi ya Tanzania, (Cape Town) South Afrika hadi (Cairo) Misri, hivyo kurahisisha huduma za  usafirishaji wa abiria na mizigo kutoka hapa kuelekea maeneo mengine", amesema Ngonyani.

Pia Naibu Waziri ameitaka kampuni ya ujenzi ya Chico kuhakikisha inamaliza daraja hilo ifikapo Oktoba mwaka huu kama ilivyoandikwa kwenye mkataba ili wananchi kuweza kulitumia.

Kwa upande wake Mhandisi Mshauri wa mradi huo, Leornado Licari, amesema kuwa kwa sasa mradi umefika asilimia 87 ambapo hivi karibuni wanatarajia kuweka lami.

"Nakuhakikishia kumaliza mradi huu kwa wakati kwani kazi zilizobaki kwa sasa hivi ni chache, kwa hiyo hadi kufikia mwezi Septemba tutakuwa tumeshakamilisha kazi zote", amesisitiza Licari.

Naibu Waziri Ngonyani yupo katika ziara ya kikazi ya siku moja katika mikoa ya Dodoma na Manyara ambapo pamoja na ukaguzi wa daraja hilo pia amekagua madaraja mengine matatu likiwemo la Msui, Kingali na Mela pamoja na ujenzi wa barabara ya Mela-Bonga KM 88.8.