VIDEO: Bunge lapewa ufafanuzi zilipo Sh1.5 trilioni

SERIKALI YATOA UFAFANUZI KUHUSU MATUMIZI YA SH 1.5 TRILIONI

Muktasari:

Wizara ya Fedha yatoa mchanganuo kuonyesha ni fedha za matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva.

Mapato tarajiwa na mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar.

Dodoma. Serikali imetoa mchanganuo wa Sh1.5 trilioni zinazodaiwa kutojulikana zilipo.

Akizungumza bungeni leo Aprili 20, 2018, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji amesema Sh697 bilioni zilitumika kwa matumizi ya dhamana na hati fungani zilizoiva; Sh687 bilioni kwa ajili ya mapato tarajiwa; na Sh203 bilioni ni za mapato ya kodi yaliyokusanywa kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar.

Dk Kijaji alitoa ufafanuzi baada ya Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kukatisha kipindi cha maswali na majibu na kuipa Serikali nafasi ya kutoa hoja ya kutoonekana kwa kiasi hicho kwenye matumizi ya Serikali katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).

Dk Tulia amesema maswali na majibu yatapangiwa utaratibu mwingine.

“Hakuna Sh1.5 trilioni iliyopotea au kutumika kwenye matumizi ambayo hayakuidhinishwa na Bunge tukufu. Madai ya watu wasiyoitakia mema nchi kuhusu matumizi ya fedha hii hayana nia njema na nchi,” amesema Dk Kijaji.

Amesema kutoonekana kwa fedha hizo kulitokana na taarifa ya ukaguzi ya CAG kutumia taarifa za hesabu za nyaraka mbalimbali, hivyo kutojumuishwa kwa baadhi ya taarifa za utekelezaji wa bajeti.

Dk Kijaji amesema hadi Juni, 2017 mapato yalikuwa Sh25.3 trilioni na matumizi yalikuwa Sh23.79 trilioni.

“Matumizi haya hayakujumuisha Sh697.85 bilioni zilizotumika kulipa dhamana na hati fungani za Serikali zilizoiva,” amesema.

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na mbunge wa Kigoma Mjini amekuwa akizungumza na waandishi wa habari na kupitia mitandao ya kijamii kueleza kuwa fedha hizo hazikutolewa kwa matumizi hivyo kutokaguliwa na CAG.