Naibu waziri apigilia msumari marufuku kuuza chakula nje

Naibu waziri wa Kilimo, Dk Mary Mwanjelwa

Muktasari:

  • Awali, marufuku ya uuzaji wa chakula nje ilitangazwa Juni 26 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za Eid, ambapo aliwataka wafanyabiashara kama wanaona kuna umuhimu wafanye hivyo baada ya kupata vibali.

Dar es Salaam. Naibu waziri wa Kilimo, Dk Mary Mwanjelwa amesema licha ya Tanzania kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 120, wakulima hawaruhusiwi kuuza mazao ya chakula nje ya nchi.

Awali, marufuku ya uuzaji wa chakula nje ilitangazwa Juni 26 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za Eid, ambapo aliwataka wafanyabiashara kama wanaona kuna umuhimu wafanye hivyo baada ya kupata vibali.

Akizungumza jana katika mkutano wa wadau wa kilimo kwa ajili ya kupunguza upotevu, kuimarisha usalama wa chakula na uanzishwaji wa viwanda uliofanyika jijini Dar es Salaam, Dk Mwanjelwa aliwataka wafanyabiashara kuangalia mikoa yenye upungufu wa chakula na kupeleka badala ya kuuza nje ya nchi.

“Mimi natoka Mbeya na ni kweli mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inalima chakula cha kutosha, lakini tuangalie kwenye mikoa mingine ya Tanzania kuna ukame hakuna chakula cha kutosha, hatuwezi kusema kwa kuwa wao wanalima chakula cha kutosha kwa hiyo tupeleke chakula nje ya nchi,” alisema na kuongeza:

“Kwa hiyo niwaombe wafanyabiashara wachangamkie fursa, waende kwenye hiyo mikoa inayolima chakula cha ziada katika ile mikoa mingine wapeleke kule, bei imeshuka.”

Alisisitiza pamoja na kushuka kwa bei ya mazao sokoni bado hairuhusiwi kuuza nje ya nchi akisema kipaumbele cha Serikali ni Watanzania kwanza. “Pamoja na kwamba bei imeshuka hatuwezi tukasema tunapeleka chakula nje ya nchi wakati hapa kwetu kuna mikoa haina chakula. Kazi yetu ni kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata chakula katika soko la ndani,” alisema Dk Mwanjelwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, katibu mtendaji wa Jukwaa la Kilimo (Ansaf), Audax Rukonge alisema mazao hupotea kutokana na kutokuwa na uvunaji bora, wakati wa kusafirisha, uhifadhi hafifu na wadudu waharibifu. “Mkakati uliopo sasa ni kupunguza upotevu huo hadi asilimia 20 ifikapo mwaka 2025. Jambo hilo lina maana hasa kwa Tanzania ya viwanda kwa sababu vinategemea mali ghafi kutoka kwenye kilimo,” alisema Rukonge.

Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Aloyce Hepelwa alisema upotevu wa chakula umesababisha nchi kuwa na njaa licha ya kuzalisha chakula kingi. “Sababu kubwa ni usafirishaji wa mazao baada ya kuvunwa na kupelekwa sehemu mbalimbali na kuhifadhiwa. Tatizo hili linasababisha kuwepo kwa njaa na kwa kuwa sasa tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda vinategemea sana mazao ya kilimo,’ alisema Dk Hepelwa.

Mkurugenzi msaidizi wa kitengo cha kuhifadhi na usindikaji wa mazao ya chakula, Josephine Amolo alisema kutokana na upotevu huo, Serikali imeanzisha kitengo hicho ili kutoa elimu kwa wakulima na wadau wa kilimo.