Tuesday, December 12, 2017

Ofisi ya damu salama yatakiwa kutanua wigo wa huduma

Naibu Waziri wa Afya Dk Faustine Ndugulile

Naibu Waziri wa Afya Dk Faustine Ndugulile akimkabidhi cheti cha ithibati ya utambuzi daraja la pili kwa Meneja wa Damu Salama kanda ya Mashariki Dk Aveline Mgasa.Picha na Elizabeth Edward 

By Elizabeth Edward, Mwananchi eedward@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile ameitaka ofisi ya Mpango wa Taifa wa Damu  Salama kutanua wigo wa huduma na kuhakikisha kila hospitali ya mkoa inakuwa na kitengo cha uchangiaji damu.

Dk Ndugulile pia, ameitaka ofisi hiyo kuendelea kuhamasisha watu kujitolea damu ili kuongeza idadi ya wachangiaji wa kudumu ambao sasa wapo 199,000.

Amesema kitengo cha utoaji damu katika kila hospitali ya mkoa kitasaidia dharura zinapojitokeza.

Dk Ndugulile amesema hayo wakati wa hafla ya kukabidhiwa vyeti vya ithibati vya utambuzi wa daraja la pili vilivyotolewa na jumuiya ya uchangiaji damu Afrika (AfSBT) kwa kanda ya Mashariki (Dar es Salaam), kanda ya Kaskazini (Moshi) na Zanzibar.

Amesema kuwepo kwa huduma hiyo kutasaidia kupunguza vifo vya wanawake vinavyotokana na kumwaga damu nyingi wakati wa kujifungua.

 “Tunapozungumzia huduma bora za afya ni lazima tuwe na uhakika wa upatikanaji wa damu salama kwa wakati. Nchi yetu ni kubwa hivyo hatuwezi kuwa tunategemea ofisi za kanda pekee  ni muhimu kuwa na kitengo cha damu katika kila hospitali ya mkoa,” amesema.

Dk Ndugulile ametaka ofisi hiyo kuhakikisha huduma za upimaji na uchangiaji wa damu zinafanyika kwa mashine za kisasa ili kupunguza uwezekano wa kutokea makosa ya kibinadamu.

Akizungumzia hilo, mkurugenzi msaidizi wa huduma za kinga, Dk Charles Massambu amesema tayari wameanza kulifanyia kazi.

 “Tupo katika mchakato wa kununua vifaa vya kisasa vya utoaji na upimaji wa damu na vimeshaanza kununuliwa, muda si mrefu shughuli zetu zitakuwa zikifanyika kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa zaidi,” amesema.

-->