VIDEO: Nape, Ghasia waliamsha bungeni ushuru wa korosho

Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Wasema kinachofanywa na Serikali kitaimaliza CCM mikoa ya Kusini


Dodoma. Wabunge wa CCM, Nape Nnauye (Mtama) na Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) wamesema hawakubaliani na mapendekezo ya Serikali ya kufuta ushuru wa asilimia 65 wa fedha zinazotokana na mauzo ya korosho nje na kubainisha kuwa kinachofanywa ni kuiua CCM mikoa ya Kusini.

Wakizungumza leo Jumatatu Juni 25, 2018 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Serikali, wamesema wapo tayari  kudhalilishwa na wabunge wenzao waliopangwa kuitetea Serikali katika suala hilo la Korosho huku mawaziri wawili wakisimama kutetea jambo hilo.

Tayari baadhi ya wabunge wametishia kufanya maandamano iwapo Serikali haitatoa asilimia 65 za ushuru wa mauzo ya korosho nje kwa ajili ya maendeleo ya zao hilo.

Pia, wanapinga mabadiliko ya Sheria ya Korosho yanayokusudiwa kufanywa na Serikali ili ushuru huo upelekwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina.

Aliyeanza kuzungumza alikuwa Nape aliyebainisha kuwa ukizungumzia korosho unazungumzia maisha ya watu katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na mingine inayolima korosho.

“Wakulima wa pamba wakizungumza pamba wanazungmza maisha, sisi hatuna mifugo, almasi na tukizungumza korosho ni maisha na linapozungumzwa hili ushabiki uwekwe pembeni, tunazungumza maisha,” amesema.

“Hili jambo tulilizungumza katika wizara ya Kilimo na mwenyekiti wa Bunge (Mussa Azzan Zungu) ulikuwapo na tulizungumza nje na hatukukubaliana.

Amebainisha kuwa dhana kuwa mapato yote ya korosho yasaidie mikoa ya Kusini si kweli, kwamba yatafanya shughuli nyingine, “badala ya kutuletea fedha unaleta sheria ya kuzifuta kabisa, huku ni kutudharau kwa hali ya juu, mimi nadhani ushauri wangu hebu zungumzieni namna ya kuleta fedha na hii sheria ondoeni kwanza.”

“Dk Mpango mbona unazungumza na korosho na katani peke yake, mbona nia ovu, unapora fedha halafu unaleta sheria hii, maisha haya ni maisha yetu. Tunaopata madhila mabaya zaidi katika gesi, mbaazi imeanguka.”

Huku akizungumza kwa uchungu Nape amesema, “Wanaosema si hela zetu hiki kiatu hamvai nyinyi tunakivaa sisi. Dk Mpango kuweni na huruma na mapendekezo haya yanakwenda kuiua CCM Kusini, yanakwenda kutuweka mahali pagumu sana.”

Kauli hiyo ilimuinua Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, mhandisi Stella Manyanya akimtaka Nape anapochangia kutowashawishi wananchi wa mikoa ya Kusini kupinga mambo mbalimbali yanayoazimiwa kufanywa na Serikali.

Kwa upande wake Ghasia ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti amesema,” kuna wabunge wamekaa vikao, wameandaliwa

waje kutudhalilisha wabunge tunaowatetea wakulima.”

“Wabunge wote tuna haki sawa za kutetea wananchi wetu, anayetoka katika pamba atetee pamba, anayetoka katika madini atatetea madini yake na anayetoka katika korosho atatetea wa korosho.’

“Niwahakikishia wakulima wanaolima korosho wabunge wao tutapambamba na hata haki isipopatikana ila tutawatetea. Tunaambiwa sisi wabinafsi, korosho inalimwa kwa kiwango kikubwa na mikoa miwili au mitatu lakini tulipokaa katika kamati tukakubaliana na kwenda mikoa 17,”

Amesisitiza, “Leo tunaambiwa sisi wabinafsi, kuna watu wanakuja kusimama wanasema wanaijua korosho kuliko sisi. Mimi utafiti wangu wa shahada ya kwanza na ya pili inahusu korosho. Leo mtu anakuja humu anaijua korosho na ninasema kila mtu atetee lake na wananchi mjiandae kuwasikia.”

Baada ya Ghasia kumaliza kuchangia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama alisema Serikali haina nia ovu na suala la korosho na haina nia ya kuwanyanyasa wakulima wa zao hilo.

Katika ufafanuzi wake kuhusu mvutano huo, mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu amesema jambo hilo lisiligawe Bunge na kuwataka wabunge kusubiri hoja zitakazotolewa na Serikali wakati ikijibu jambo hilo.