Nape apata ajali ya gari

Muktasari:

  • Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye leo asubuhi Septemba 24, 2018 amepata ajali ya gari akitokea Mtwara kwenda Lindi, hakuna aliyejeruhiwa katika ajali hiyo

Lindi/Dar. Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amepata ajali ya gari eneo la kijiji cha Kibutuka wilayani Liwale mkoani Lindi.

Ajali hiyo imetokea asubuhi ya leo Septemba 24, 2018 akiwa njiani kutoka Mtwara kwenda Liwale kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Lindi.

Katika gari, Nape aliyewahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo alikuwa na watu wengine ambao ni Josephin Kibiriti mwandishi wa Star Tv, Mohamed Chiwalo ambaye ni Katibu Mwenezi wa CCM wilyani Nachingwea na msaidizi wake.

Kamanda wa polisi mkoa wa Lindi, Prodecina Protas amesema amepokea taarifa ya ajali hiyo na jeshi la polisi linafanya uchunguzi ili kujua chanzo cha ajili.

Akizungumza na Mwananchi, Nape amesema katika ajali hiyo hakuna aliyejeruhiwa.

“Ni kweli tumepata ajali wakati tunatoka Mtama kwenda Liwale kuhudhuria mkutano wa halmashauri kuu ya CCM mkoa, lakini wote tuko salama na hapa tunasubiri gari jingine linakuja kutuchukua,” amesema Nape.

Mbunge huyo amebainisha kwamba hakuna majeruhi kwenye ajali hiyo na wanaendelea na safari kwenda kwenye mkutano huo.